Mbinga. Katika juhudi ya kutekeleza agizo la utoaji wa vyakula vyenye virutubisho shuleni, Halmashauri ya Mji wa Mbinga (MTC) jana Agosti 17 ilifanya kikao na wamiliki wa mashine za kuzalisha unga pamoja na SANKU---mtoa huduma katika programu ya kuchanganya virutubishi kwenye unga wa mahindi.
Kikao kilicho wakutanisha SANKU pamoja na wamiliki wa mashine za nafaka kutoka kata nane za Mbinga Mji kililenga kihamasisha wana Mbinga Mji kuwa na mashine nyingi za kuchanganya virutibishi kwenye unga wa mahindi.
Akizungumza wakati wa kikao msimamizi wa kanda wa SANKU Christian Lutaja alisema mashine na virutubishi hotolewa bure na kwamba wahitaji wanachotakiwa kufanya ni kununua mifuko tuu.
"Oda ya kwanza inatakiwa isipungue mifuko 2,000," alisema bwana Lutaja.
Alisema mfuko wa kilo 5 huuzwa kwa Sh475, wakati kilo 50 ni Sh900.
Katika mkoa wa Ruvuma tayari mashine 30 za kuchanganya virutubishi kwenye unga wa mahindi zimefungwa huku Halmashauri ya Mji wa Mbinga ikiwa ni mashine tatu, kwa mujibu wa Lutaja.
Taarifa za uwepo wa kikao na SANKU zilitolewa jana asubuhi na kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji wa Mbinga Dkt Kung'e Nyamuryekung'e wakati wa kikao cha kamati kuhusu taarifa ya utekelezaji wa shughuli za lishe Robo ya nne ya 2022/23 kilichofanyika MTC.
"Tunataka kuhamasishana na kuwapa elimu kuhusu umuhimu wa kufunga mashine hizo za kuongeza viini lishe," alisema Dkt Nyamuryekung'e ambaye pia ni mkuu wa Idara ya Huduma za Afya, Ustawi wa Jamii na Lishe katika halmashauri ya Mji wa Mbinga.
Alisema uamuzi huo ni utekelezaji wa moja ya maazimio ya kikao cha kamati ya lishe ngazi ya halmashauri kilichofanyika Agosti 6 mwaka huu.
Aliongeza kuwa katika kikao hicho ilibainika kuwa utoaji wa vyakula vyenye virutubisho shuleni ni changamoto kwasababu mashine za kuongeza viini lishe ni chache.Kutokana na changamoto hiyo, kamati iliadhimia kuwa wananchi wahamasishwe kulima mazao yenye viini lishe ili watoto wale vyakula vyenye lishe.
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 S.L.P 74,SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: 0252602256
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.