MKURUGENZI Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya Mbinga mkoani Ruvuma Juma Mnwele amesema wilaya hiyo imeamua kuanzisha shule maalum ya wavulana(Mbinga Boys) baada ya kupata mafanikio makubwa katika shule dada ya wasichana (Mbinga Gilrs).
Akitoa taarifa ya mradi huo kwa Kamati ya Siasa ya CCM Mkoa wa Ruvuma Mnwele amesema shule hiyo inaendelea kujengwa katika kijiji cha Ndongosi,na kwamba hatua za usajili wa shule hiyo zinaanza Oktoba mwaka huu ili mapema Januari 2021 shule ianze kupokea wanafunzi.
Amesema shule hiyo itapokea vijana wa kiume wawili waliofaulu vizuri kutoka katika kila kata wilayani Mbinga na kwamba lengo la mradi huo ni kuwa na shule bora ya wavulana na yenye ufaulu mzuri kama ilivyo kwa shule ya sekondari ya wasichana ya Mbinga iliyojengwa eneo la Mkako barabara kuu ya Songea-Mbinga.
“Shule hii itaongeza idadi ya wanafuzi wenye vipaji wanaokwenda kupata elimu ya sekondari,shule itakuwa na mazingira bora ya kujifunzia na kufundishia ili kuifanya elimu kwa vijana wetu kuwa bora na yenye tija’’,alisisitiza Mkurugenzi.
Akizungumzia gharama za mradi wa sekondari hiyo,Mkurugenzi huyo amesema hadi sasa zimetumika shilingi milioni 70 kutekeleza mradi huo zilizotoka kwa wadau mbalimbali wakiwemo Kampuni ya uchimbaji wa madini TANCOAL waliotoa sh.milioni 20 na shilingi milioni 50 zimetolewa na Halmashauri.
Amesema katika awamu ya kwanza ya ujenzi umehusisha vyumba vitatu vya madarasa kwa gharama ya sh.milioni 20,ambapo katika awamu ya pili iliyogharimu sh.milioni 50 umehusisha ujenzi wa maabara,ukarabati wa nyumba ya Mwalimu Mkuu,ukarabati wa hosteli,ukarabati wa vyumba sita vya madarasa na ujenzi wa vyoo vya walimu na wanafunzi.
Kulingana na Mnwele madarasa sita kila moja lina uwezo wa kuchukua wanafunzi 40 ambapo madarasa yote yatakuwa na uwezo wa kuchukuwa wanafunzi 240 na kwamba hadi sasa madarasa matatu yamekamilika kwa asilimia 85,madarasa matatu yamefikia asilimia 60,nyumba ya Mkuu wa shule na hosteli imefikia asilimia 80.
Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Mbinga Cosmas Nsenye akizungumzia mradi huo,amesema Halmashauri zote mbili za wilaya hiyo ambazo ni Mbinga Mji na Halmashauri ya Wilaya zina ushirikiano mkubwa hali ambayo imesababisha kuwa na shule mbili maalum za wasichana na wavulana.
“Naomba Wilaya na Halmashauri nyingine nchini waige mfano wa wilaya ya Mbinga kwa kuanzisha sekondari za vipaji maalum ndani ya Halmashauri husika,hizi ni sekondari za bweni ambazo zina mazingira rafiki ya kujifunzia na kufundishia’’,alisisitiza Nsenye.
Kwa upande wake Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM Taifa Musa Homera akizungumza mara baada ya kukagua shule hiyo ameupongeza uongozi mzima wa Halmashauri hiyo kwa kuanzisha shule hiyo ambayo itasaidia kuboresha elimu kwa watoto .
Amesema serikali ya awamu ya tano inayoongozwa na Rais Dkt.John Magufuli katika kipindi cha miaka mitano imepata mafanikio makubwa katika ujenzi wa miundombinu mbalimbali ikiwemo ya shule.
“Tangu mwaka 1961 tumepata uhuru,katika kipindi cha miaka mitano hii kuanzia mwaka 2015 hadi 2020,miradi iliyotekelezwa Tanzania karibu inalingana na miradi iliyoanzishwa kuanzia mwaka 1961 hadi mwaka 2015,Rais wetu amefanyakazi kubwa sana’’,alisisitiza Homera.
Imeandikwa na Albano Midelo
Afisa Habari wa Mkoa wa Ruvuma
Julai 7,2020
Mbinga
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 S.L.P 74,SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: 0252602256
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.