MKUU wa Mkoa wa Ruvuma Christina Mndeme amesema zao la korosho ni msingi wa uchumi katika Mkoa wa Ruvuma.
Mndeme ametoa kauli hiyo wakati anafungua mkutano wa wadau wa korosho wa Mkoa wa Ruvuma uliofanyika mjini Tunduru ambapo mnada wa kwanza wa korosho umetangazwa kufanyika Oktoba 22 mwaka huu.
Mndeme amesema Mkutano huo wa wadau wa Korosho kwa Mkoa wa Ruvuma unalengo la kujadili na kutoa mapendekezo mbalimbali kutokana na changamoto zinazolikabili zao la Korosho na Sekta ya Korosho kwa ujumla.
“Wilaya zinazolima Korosho kwa uchache waongeze hamasa ya uzalishaji ili nao waweze kulingana na Wilaya zinazolima korosho kwa wingi pamoja na uanzishaji wa mapya utawezesha kuchangia lengo la Serikali ya Tanzania uzalishaji wa Korosho ghafi toka wastani wa tani 300,000 hadi tani 1,000,000 ifikapo mwaka 2025” alisema Mndeme.
Mndeme ametoa wito kwa bodi ya Korosho Tanzania kuendelea kuhamasisha maendeleo ya zao la korosho hapa nchini kupitia bajeti ya Serikali kuwa na mashamba mapya ya uzalishaji na yale ya asili yanayozingatia kilimo bora cha zao hilo na kinacholeta tija.
Ametoa rai kwa wadau wa korosho kuongeza uzalishaji na kupanua wigo wa soko kwa ubanguaji wa Korosho ili kuongeza thamani ya zao hilo ambapo amesema hivi sasa korosho zinazobanguliwa katika Mkoa wa Ruvuma ni asilimia ishirini ya zinazovunwa nchini.
Ameagiza kuweka mikakati itakayoweza kuboresha zao hilo ikiwemo kuhakikisha upatikanaji wa mitaji kwa wabanguaji wadogo,wakati na wakubwa pamoja na kupanua wigo wa soko la korosho.
“Serikali ya awamu ya tano chini ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt.John Magufuli ina mpango wa kuona wakulima wanapata bei nzuri ya mazao yao kulingana na bei ya soko,ina nia ya dhati kuhakikisha kiasi kikubwa cha korosho inayozalishwa hapa nchini inabanguliwa na viwanda vya ndani”,alisema Mndeme.
Imeandaliwa na Aneth Ndonde
Kutoka ofisi ya Habari ya Mkoa wa Ruvuma
Oktoba 3,2020
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: 0252602256
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.