TAMASHA la kumbukizi ya miaka 114 ya vita ya Majimaji linafanyika kwa siku sita katika viwanja vya Makumbusho ya Taifa ya Majimaji mjini Songea.
Mhifadhi wa Makumbusho ya Taifa ya Majimaji Adson Ndyanabo amesema tamasha hilo linaanza Februari 22 na kilele chake kinatarajiwa kuwa Februari 27 mwaka huu na kwamba katika tamasha hilo wadau watashiriki maonesho ya vyakula vya asili ya Mkoa wa Ruvuma.
Shughuli nyingine zitakazofanyika kwenye tamasha hilo amezitaja kuwa ni kazi za sanaa za mikono,maonesho ya vita ya Majimaji,mavazi ya asili,burudani za ngoma za asili,muziki na kufanyika magwaride ya heshima.
Ndyanabo ameitaja kaulimbiu katika tamasha la mwaka huu kuwa ni Maisha ya wazee wetu fahari yetu na kwamba mgeni rasmi kenye kilele cha tamasha hilo Februari 27 anatarajiwa kuwa Waziri Mkuu wa Tanzania Kassim Majaliwa.
Hata hivyo amesema tamasha hilo linatarajiwa kuzinduliwa na Waziri wa Maliasili na Utalii Dkt.Damas Ndumbaro sanjari na kuzindua vilabu vya Historia na uzalendo vilivyoanzishwa katika shule ikiwa ni utekelezaji wa agizo la Rais Dkt.John Magufuli kuhakikisha vijana mashuleni wanapata elimu ya uzalendo na historia ya nchi kwa ujumla.
Amesema tamasha hilo pia linafanya kongamano la wadau kwa lengo la kupeana elimu,mila na utamaduni wa Mkoa wa Ruvuma na Taifa kwa ujumla.
Akizungumzia historia ya Makumbusho ya Taifa ya Majimaji,Mhifadhi huyo amesema Makumbusho ya Taifa ya Majimaji yaliyopo Mahenge mjini Songea,ni miongoni mwa makumbusho saba ya Shirika la Makumbusho ya Taifa na vituo 91 vya kale vilivyopo nchini.
“Makumbusho ya Majimaji yalianzishwa na kufunguliwa Julai 6,1980, na aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Dkt.Lawrence Gama,lengo la kuanzisha makumbusho hayo ni kutunza kumbukumbu ya historia ya vita ya Majimaji iliyoanza mwaka 1905 hadi 1907’’,alisisitiza.
Amesema Makumbusho hiyo imejengwa katika eneo ambalo mashujaa 67 walizikwa baada ya kunyongwa kikatili na wajerumani.
Amelitaja eneo hilo la mashujaa maarufu kama hero square kuwa kuna makaburi mawili ya mashujaa moja ni la halaiki ambalo wamezikwa mashujaa 66 katika kaburi moja baada ya kunyongwa na serikali ya wakoloni wa kijerumani Februari 27,1906.
Kwa mujibu wa Mhifadhi huyo,kaburi la pili lililopo kwenye makumbusho hayo ni la Jemedari wa wangoni,Nduna (Sub chief) Songea Mbano aliyenyongwa Machi 2,1906 na kwamba Mji wa Songea umepewa jina la jemedari huyo.
Imeandikwa na Albano Midelo
Afisa Habari Mkoa wa Ruvuma
Februari 22,2021
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: 0252602256
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.