Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Kanali Ahmed Abbas Ahmed amesema serikali inatekeleza miradi mikubwa ya maendeleo katika Mkoa wa Ruvuma ikiwemo ujenzi wa hospitali ya Rufaa ya Mkoa ambayo ujenzi wake unaendelea katika eneo la Mwengemshindo Manispaa ya Songea.
Akizungumza na wananchi wa Kata ya Ruvuma Manispaa ya Songea kwenye tamasha la JIKUNE lililoandaliwa na Kituo cha redio cha Selous FM,Kanali Abbas amesema hospitali ya Rufaa ya Mkoa licha ya kutumiwa na wananchi wa Mkoa wa Ruvuma,pia inaweza kutumiwa na wananchi kutoka nchi Jirani za Msumbiji,Malawi na Komoro.
Ameitaja baadhi ya miradi iliyotekelezwa katika sekta ya afya kuwa ni ujenzi wa zahanati,hospitali za wilaya, nyumba za watumishi,ununuzi wa vifaa na vifaatiba vya kisasa ambapo hivi sasa kuna xray na CT Scan kubwa na za kisasa hivyo kurahisisha matibabu na kuokoa Maisha.
Ameitaja miradi mingine ya kimkakati inayoendelea kutekelezwa mkoani Ruvuma kuwa ni ujenzi wa barabara ya lami kutoka Kitai- Ruanda wilayani Mbinga hadi Lituhi wilayani Nyasa.
“Barabara hiyo licha ya kutumika kusafirisha watu,lakini pia itasaidia usafiirishaji katika migodi mikubwa ya makaa ya mawe ya Kampuni za JITEGEMEE,TanCoal na Ruvuma Coal kwa sababu kwa kiwango kikubwa makaa ya mawe ni lazima yasafirishwe Kwenda kwenye bandari zetu za Mtwara,Dar es salaam na Tanga ili yaweze Kwenda nje ya nchi na kuiwezesha serikali kupata mapato’’,alisema Kanali Abbas.
Akizungumzia mradi wa utoaji mbolea ya ruzuku,Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma amesema mbolea hiyo ikitumiwa vizuri itawezesha kuzalisha chakula cha kutosha ndani ya Mkoa na ziada Kwenda kuuzwa kwa majirani zetu na mikoa mingine.
Amesisitiza kuwa Mkoa wa Ruvuma gwiji la uzalishaji wa mazao ya nafaka na kwamba Mkoa unafahamika kama ghala la chakula la Taifa kutokana na kuongoza kitaifa katika uzalishaji.
Katika sekta ya elimu Mkuu wa Mkoa amesema serikali imetoa fedha kutekeleza ujenzi wa shule na madarasa katika shule za awali,msingi, sekondari,ujenzi wa nyumba za walimu na kwamba katika Mkoa wa Ruvuma serikali imetoa fedha za kujenga sekondari maalum ya wasichana ya Mkoa wilayani Namtumbo.
Sekondari hiyo ambayo imesajiriwa jina la Dkt.Samia Suluhu Hassan imeanza kuchukua wanafunzi wa kike wa kidato cha tano na kwanza ambapo hadi sasa serikali imetoa Zaidi ya shilingi bilioni nne kutekeleza mradi huo.
Akizungumzia sekta ya kilimo,Kanali Abbas amesema Mkoa umezindua mnada wa kwanza wa ufuta,mnada ambao umefanyika kwa kutumia teknolojia ya kidijitali inayomwezesha mnunuzi kuomba kununua ufuta hata akiwa nje ya Mkoa.
Amebainisha kuwa mfumo huo humwezesha mtu kununua mazao akiwa Ulaya au Mkoa wowote na kwamba uzinduzi huo wa mfumo umeonesha bei nzuri ya mazao ya mkulima kwa sababu mfumo unaanza na bei elekezi na baadaye mnunuzi ananunua kulingana bei iliyoanza kutamkwa na Wizara ya Kilimo.
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: 0252602256
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.