KAMA unadhani jiwe la Mwanza lililopo katika ziwa Viktoria ndiyo kivutio pekee cha utalii katika maziwa hapa nchini utakuwa unajidanganya.
Katika ziwa Nyasa Mkoa wa Ruvuma kuna jiwe linaloitwa Pomonda ambalo linavivutio lukuki vya utalii ambavyo vinavutia wengi waliobahatika kufika katika jiwe hilo.Jiwe la Pomonda lenye ukubwa wa robo hekari ambalo lipo meta takribani 300 ndani ya ziwa Nyasa kutoka bandari ya Liuli.
Muongozaji watalii katika bandari ya Liuli Joseph Ndomondo ambaye pia ni Mmiliki wa fukwe ya Pomonda anasema Jiwe la Pomonda ambalo wajerumani walilipa jina la sphinxhaven kutokana na kuwa na vivutio lukuki.
Utalii wa kihistoria ni aina ya kwanza ya utalii ambayo inapatikana katika jiwe hilo ambapo tangu vita ya kwanza ya dunia mwaka 1914 hadi 1918 na vita ya pili ya dunia mwaka 1939 hadi 1945 wakoloni walitumia jiwe hilo kujificha.
Anasema wajerumani na waingereza walitumia pango kubwa lililopo katika jiwe la Pomonda ambalo lipo kama ukumbi wenye kubeba watu kati ya 60 hadi 100 hivyo wanajeshi wa kiingereza na kijerumani walitumia jiwe hilo kama sehemu ya kujificha wakati wa mapambano.
Katika jiwe hilo inaaminika kuna sahihi ya Dk.David Livingstone Mvumbuzi maarufu ambaye alivumbua milima Livingstone ambayo pia imepewa jina lake kuzunguka ziwa Nyasa.
Dk.Livingstone alizaliwa huko Blantyre,Uingereza Machi 19 mwaka 1813.Alisoma masomo ya udaktari wa binadamu katika Chuo Kikuu cha Cambridge.Alifanya safari za kuja Afrika mara tatu kwa nyakati tofauti.
Ilikuwa ni mwaka 1866 ambapo Dr. Livingstone alikuja Afrika kwa mara ya tatu.Lengo la safari yake lilikuwa ni kuchunguza chanzo cha mto Nile.Safari yake ilianzia katika chanzo cha mto Ruvuma, Mikindani Mtwara hadi ziwa Nyasa, Banguela na Mweru.
Uchunguzi ambao umefanywa katika Jiwe la Pomonda umebaini kuwa kilele cha jiwe hilo ambacho kina urefu wa takribani meta 40 kwenda juu ipo taa maalum kubwa yenye rangi nyekundu ambayo ilikuwa itatumiwa na nchi tatu za Tanzania,Malawi na Msumbuji.
Taa hiyo ilitumika wakati wa wakoloni wa kijerumani,kireno na waingereza kwa ajili ya alama ya kuongozea meli katika ziwa Nyasa ili wasiweze kupotea wanapotaka kutia nanga kwenye bandari ya Liuli,taa hiyo iliwawezesha kuiona bandari ya Liuli hata wakiwa katika nchi za Malawi na Msumbiji.
Kivutio kingine cha utalii ambacho kinapatikana katika eneo la jiwe hilo ni mawe matatu makubwa ambayo wakazi wa eneo hilo wanaamini yamepangwa na Mwenyezi Mungu ,huku mpangilio wake ukiwa ni kivutio cha ajabu utadhani yamejengwa na mafundi ujenzi huku yakiwa yameacha njia maalum ambayo unaweza kupita kwa mtumbwi au boti kutokea upande wa pili hali ambayo inawashangaza na kuwavutia wengi.
Jiwe la Pomonda pia ni sehemu muhimu ambayo inafaa kufanya utalii wa michezo ya kwenye maji(water sports) kwa mfano mchezo wa kupiga mbizi na kuruka toka juu ya jiwe la Pomonda hadi ziwani umbali wa karibu mita 30.
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 S.L.P 74,SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: 0252602256
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.