Mstahiki Meya Manispaa ya Songea Michael Mbano ameongoza mamia ya Wananchi Manispaa ya Songea katika kuadhimisha siku ya Malaria Duniani ambayo huadhimishwa duniani kote kila mwaka ifikapo tarehe 25 aprili yaliyofanyika katika viwanja vya shule ya msingi matarawe yaliyoambatana na zoezi la upimaji BURE wa Malaria ambapo watu 88 walipata kupimwa kati ya hao watu 3 walikutwa na malaria na kupewa matibabu.
Mbano ambaye pia ni Mwenyekiti wa Baraza la Madiwani Manispaa ya Songea katika hotuba yake iliyosomwa viwanjani hapo alisema” ushiriki hafifu wa jamii katika kuboresha mazingira ya makazi na kutoondoa mazalia ya mbu ni chanzo kikuu cha ongezeko la maambukizi ya malaria kwa jamii.”
Alisema lengo la Serikali katika kuadhimisha maadhimisho haya kwa ajili ya kufanya ufuatiliaji, usimamizi, na tathimini ya mwenedo wa ugonjwa wa malaria ambao kwa mwaka 2020 hali ya maambukizi Manispaa ya Songea ni asilimia 5.9% ikiwa Kimkoa ni asilimia 11% na Kitaifa ni asilimia 7%.
Aliongeza kuwa, baadhi ya tabia za jamii kutokuchukua hatua za haraka za kupata matibabu kwenye vituo vya kutolea huduma za afya, kutozingatia matumizi sahihi ya vyandarua, na kutopata vipimo vya malaria kabla ya matibabu ni moja ya changamoto ambazo hukwamisha mapambano dhidi ya malaria.
Amewataka wananchi hao kuboresha mazingira yao ya makazi kwa kufanya usafi wa mazingira na ujenzi wa nyumba bora, kuwahi matibabu mara waonapo dalili za ugonjwa, kupata vipimo vya malaria kabla ya matibabu kwani sio kila homa ni malaria.
Katika kupambana na malaria Mstahiki Meya manispaa ya Songea, amegawa chandarua 20 kwa watu wenye mahitaji maalumu waishio katika kata ya Matarawe Manispaa ya Songea.
Ametoa Rai kwa wataalamu wa Manispaa ya Songea kufanya kazi kwa weredi sambamba na kutoa elimu kwa jamii juu ya kubadili tabia zinazochangia maambukizi ya ugonjwa wa Malaria kwa kutumia wahudumu wa afya ngazi za mitaa kwa kushirikiana na wataalamu wa idara ya afya, kutoa tiba ya tahadhari kwa wa mama wajawazito wahudhuriapo kiliniki pamoja na kuendelea kuchukua hatua za kisheria kwa wakazi wanaokiuka taratibu, kanuni na sheria za Afya na ustawi wa mazingira.” Mbano alisisitiza”.
Naye Mratibu wa Malaria Manispaa ya Songea Maxensius Mahundi alisema Malaria ni miongoni mwa magonjwa 10 yanayoongoza kwa matibabu ya nje na ndani kwa watoto walio chini ya miaka mitano 5 na akinamama wajazito.
Akizitaja dalili za ugonjwa huo ni pamoja na homa,maumivu ya viungo, mwili kulegea, kichwa kuuma, baridi na kutetemeka mwili, kutapika, kuharisha, maumivu ya kifua, kukosa hamu ya chakula, kuvimba wengu, kuvimba bandama, degedege na upungufu wa damu.
Mahundi alibainisha kuwa mwaka 2020 Manispaa ya Songea walioripotiwa kuugua ugonjwa wa malaria na kupata matibabu nje ni 19,929 sawa na asilimia 7.2% ya wagonjwa wote 276,063 waliopata matibabu nje, aidha waliolazwa kwa ugonjwa wa Malaria mwaka 2020 ni 1,785 sawa na asilimia 11.7% ya wagonjwa wote 15,219 waliolazwa.
Aliongeza kuwa watoto chini ya miaka 5 walioripotiwa ugonjwa wa malaria na kutibiwa kwa matibabu ya nje ni 5,976 sawa na asilimia 2.2 ya wagonjwa 270,087 ya waliotibiwa magonjwa mengine pia watoto chini ya miaka 5 waliopata matibabu ya ndani 3,846 kati ya hao watoto 645 walitibiwa na kulazwa kwa ugonjwa wa malaria sawa na asilimia 16%.
Vifo vilivyoripotiwa dhidi ya ugonjwa wa malaria mwaka 2020 ni 11 sawa na asilimia 37.9% ya vifo vyote 29 vilivyoripotiwa kwa magonjwa mengine. Vifo vya Watoto chini ya miaka mitano ni vifo 5 sawa na asilimia 62.5% ya vifo vyote 8 vya watoto chini ya miaka mitano.
Mahundi alifafanua kuwa hali hiyo inatokana na baadhi ya wakazi wa Manispaa ya Songea kutofuata maelekezo ya matumizi sahihi ya vyandarua, kutopima kwa uthibitisho, kutozingatia matibabu sahihi, na akina mama wajawazito kutowahi kliniki mara anapohisi kuwa ana ujauzito pamoja na kuchelewa kupata tiba za tahadhari.
Ili kukabiliana na changamoto hizo, Manispaa ya Songea imeweka mpango wa kupulizia dawa za kuuwa viluilui vya mbu kwenye mazalia ya mbu ambapo kwa mwaka 2020 Manispaa ya Songea ilipulizia mazalia ya mbu mita za mraba 11088, pamoja na kuendelea kusambaza chandarua mashuleni kila mwaka mbapo 2020 viligawiwa vyandarua 19,860 kwa shule za Msingi 85 kwa darasa la 1,2,3,5 na la 7 pamoja na uendeshaji wa usafi kila mwisho wa mwezi.
Akitoa shukrani kwa wadau wa mashirika yasiyo ya kiserikali PSI, MSD kupitia kampuni ya Simba Logistic katika kupambana na ugonjwa malaria Manispaa ya Songea.
Kauli mbiu ya mwaka 2021 ya Maadhimisho ya siku ya Malaria Duniani ni;
“ZIRO MALARIA INAANZA NA MIMI, NACHUKUA HATUA KUITOKOMEZA”.
Imenadikwa na Amina Pilly
Afisa Habari Manispaa ya Songea
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: 0252602256
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.