Na Albano Midelo
Ukitafuta mahali pa kutuliza akili, kukutana na historia ya kweli, kushuhudia maajabu ya maumbile, na kusikia sauti ya asili ikizungumza na moyo wako, basi jibu lipo katika Msitu wa Hifadhi ya Matogoro Mashariki.
Takriban kilomita 15 kutoka katikati ya Manispaa ya Songea mkoani Ruvuma, unapokaribia milima ya Matogoro, upepo unaanza kubeba harufu ya miombo, milio ya ndege wa porini na upekee wa mazingira ambayo hayajaguswa na mikono ya uharibifu.
Huu si msitu wa kawaida ni nyumba ya historia, chemchemi ya mito mikuu, na mahali ambapo roho ya vita ya Majimaji bado inanong’ona kwenye mapango ya matambiko.
Mlima Uliojaa Hazina ya Kipekee
Kwa mujibu wa Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS), Msitu wa Matogoro Mashariki ulitangazwa rasmi kuwa Hifadhi ya Taifa mnamo Novemba 6, 1951 kwa Tangazo la Serikali Na. 260. Awali ulikuwa na ukubwa wa hekta 3,533, lakini baada ya upimaji mpya sasa unaenea kwa hekta 7,457, ukiwa ni moja ya maeneo makubwa zaidi ya hifadhi ya asili mkoani Ruvuma.
Msitu huu unajumuisha milima mikubwa yenye miteremko mikali, mabonde ya kina, na vilele vya mawe vilivyopo kati ya mita 1,800 hadi 2,150 kutoka usawa wa bahari. Kilele chake cha juu kipo kwenye urefu wa mita 2,051, na ndiyo sehemu ya juu kabisa katika mkoa wa Ruvuma – kivutio kikubwa kwa wapenda mandhari na wapiga picha wa asili.
Chanzo cha Mito Mikuu na Uhai wa Maelfu
Msitu wa Matogoro unashangaza. Hapo ndipo Chanzo cha Mto Ruvuma kinapopatikana — mto unaoelekea Bahari ya Hindi na kutenganisha Tanzania na Msumbiji.
Pia kuna Mto Luhira unaotiririsha maji hadi Ziwa Nyasa. Ndani ya msitu huo, kuna mito midogo kama Liwoyowoyo, Lipasi, Mkurumusi, Limbyanda, na Masumela, yote ikianza safari yake kutoka vyanzo vya milimani baraka kwa wakazi wa mabondeni wanaotegemea kwa kilimo, malisho na matumizi ya nyumbani.
Aina Adimu za Viumbe na Mimea
Matogoro si tu msitu ni hifadhi ya maisha. Kuna misitu ya miombo, msitu wa mito, na hata mashamba ya miti ya kupandwa. Ndani yake wanaishi wanyama kama pundamilia wa milimani (klipspringers), digidigi, nyani, tumbili na hata chui. Wanyama wakiwemo mamba , chatu, swila, na kobra pia hupatikana. Aidha, ndege wa kuvutia kama vipanga na tai huruka juu ya miti kwa mandhari ya kupendeza.
Mapango ya Vita na Matambiko
Juu ya kivutio cha asili, Matogoro ni nyumba ya historia. Kuna mapango yaliyotumiwa na wapiganaji wa Majimaji kati ya 1905 hadi 1907, walipojificha na kujiandaa kwa mapambano dhidi ya ukoloni wa Kijerumani. Leo hii, mapango haya bado yanatumika kwa shughuli za matambiko ya kimila yakihifadhi roho za mababu na hadithi za kishujaa zisizopaswa kusahaulika
Shughuli Bora za Utalii
Kama wewe ni mpenzi wa utalii wa kiikolojia, Matogoro ndiyo paradiso yako. Wageni wanaweza kufanya:Safari za kutembea kwa miguu (walking safaris),Kupanda milima (hiking),Kutazama ndege (bird watching),Shughuli za kitamaduni na matambiko,Picha za kipekee (photographic safaris),Sherehe na matamasha (ceremonies & festivals) na Elimu ya mazingira (eco-education)
Bei za kuingia Kwa Mtanzania ni Tsh 3,000 tu kwa mtu mzima, watoto ni nusu bei, na watoto chini ya miaka 5 ni bure kabisa. Kwa wageni wa nje, ni Tsh 30,000 thamani ndogo kwa utajiri mkubwa wa asili.
Matogoro ni Zaidi ya Msitu – Ni Nyumba ya Uhai na Historia
Matogoro si tu kivutio cha kijiografia — ni kiini cha uhai, kumbukumbu ya ukombozi, na shule ya asili kwa kizazi cha sasa na kijacho. Ni mahali ambapo historia ya Majimaji inakutana na chemchemi ya mito mikuu, mahali ambapo utalii unavikwa taji la maana halisi ya urithi wa taifa.
Katika enzi hii ya maendeleo ya haraka, kuna kila sababu ya kuilinda Matogoro sio kwa ajili ya sisi pekee, bali kwa vizazi vijavyo, ambavyo navyo vinapaswa kujifunza kupumua hewa ya usafi wa Matogoro, kusikiliza sauti ya mito yake, na kuandika historia mpya ya utalii wa Tanzania.
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 S.L.P 74,SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: KERO PIGA 0800110174
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.