MKUU wa Mkoa wa Ruvuma Brigedia Jenerali Wilbert Ibuge amezindua maadhimisho ya siku ya mbolea duniani yaliyofanyika katika uwanja wa Majimaji mjini Songea.
Kabla ya kuzindua maonesho hayo RC Ibuge alikagua vibanda 41 vya washiriki wa maonesho ambayo yanafanyika kuanzia Oktoba 11 na kilele chake ni Oktoba 13.
Akizungumza na wananchi kwenye uzinduzi huo Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma,amesema Mkoa una chakula cha kutosha kwa muda mrefu ambapo katika msimu wa mwaka 2020/2021,Mkoa wa Ruvuma umezalisha tani 1,384,705 za mazao yote ya chakula na kuwa na ziada ya tani 894,960.
‘’Kwa zao la mahindi pekee uzalishaji ni tani 816,242 hivyo kuwa na ziada ya jumla ya tani 326,497 za mahindi’’,alisisitiza RC Ibuge.
Hata hivyo Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma,amesema uzalishaji huo unaambatana na matumizi ya pembejeo bora ikiwemo mbolea .
Ameyataja mahitaji ya mbolea katika Mkoa wa Ruvuma kuwa ni jumla ya tani 50,521 kwa msimu wa kilimo wa mwaka 2020/2021 ambapo mbolea zilizoingia na kutumika ni tani 43,000 na kwamba katika msimu wa kilimo wa mwaka 2021/2022 Mkoa unatarajia kutumia mbolea tani 50,521 za aina zote za mbolea.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya udhibiti wa Mbolea Tanzania (TFRA) Dkt.Stephano Ngailo ameutaja mkakati mkuu wa serikali ni kuhakikisha kuwa mbolea inapatikana kwa wingi na bei nafuu kwa kuwekeza kwenye ujenzi wa viwanda vya mbolea hapa nchini.
Amesema serikali imeanza ujenzi wa kiwanda cha mbolea mkoani Dodoma ambacho kitakuwa na uwezo wa kuzalisha mbolea za aina mbalimbali zaidi ya tani laki sita kwa mwaka.
Dkt.Ngailo amesema kiwanda hicho kinatarajia kuanza uzalishaji msimu wa mwaka 2022/2023, ambacho amesema kitakuwa ni ukombozi mkubwa kwa wakulima hapa nchini wakiwemo wa Mkoa wa Ruvuma ambao wanaongoza kwa kuzalisha mazao ya chakula nchini.
Kauli mbiu ya mwaka huu ya siku ya mbolea duniani ni tumia mbolea bora, kwa tija na kilimo endelevu.
Imeandikwa na Albano Midelo
Afisa Habari Mkoa wa Ruvuma
Oktoba 11,2021
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 S.L.P 74,SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: 0252602256
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.