Na Albano Midelo
Ukitaka kushuhudia maajabu ya asili, historia ya ukombozi wa Afrika, na uzuri wa utalii wa kipekee unaovutia kwa macho na roho, basi safari yako lazima ipitie Mto Ruvuma ,mto mrefu kuliko yote Afrika Mashariki na kati.
Mto Ruvuma ni mto ambao haupokei sifa kwa ukubwa wake pekee, ukiwa na urefu wa zaidi ya kilomita 800 na upana wa hadi mita 500 – bali kwa , mazingira ya kuvutia, na nafasi yake muhimu katika maendeleo ya utalii na maisha ya watu kanda ya kusini.
Chanzo Kidogo, ukubwa wa kushangaza
Kama simulizi ya hadithi za kale, chanzo cha Mto Ruvuma kipo katika milima ya Matogoro, Manispaa ya Songea mkoani Ruvuma.
Kisima kidogo tu kilicho meta 1500 kutoka usawa wa bahari. Lakini kutoka hapo, mfereji huo mdogo huanza safari ya kuandika historia katika wilaya zote tano za Mkoa wa Ruvuma: Songea, Mbinga, Nyasa, Namtumbo na Tunduru.
“Chanzo hiki si tu cha kijiografia bali pia ni ushahidi wa maajabu ya Mungu,” anasema Deborah Mwakanosya, Mratibu wa Utalii Kanda ya Kusini. “Kisima kidogo kinachobeba mto mkubwa wa kimataifa “
Mto wa Uzima na Maendeleo
Mto Ruvuma si mto tu wa kupendezesha mandhari; ni moyo unaodunda katika miradi ya maendeleo. Katika shamba la AVIV, Songea.
Maji ya mto Ruvuma yanatumika kumwagilia kahawa ,mazao ya biashara yenye thamani kubwa na kutoa ajira kwa zaidi ya watu 3,000.
Mbali kidogo, katika eneo la Tulila wilayani Mbinga, shirika la watawa wa Mtakatifu Agnes Chipole wilayani Songea,linatumia maporomoko ya mto huo kuzalisha umeme.
Mradi huo wa hydro-power unazalisha hadi megawati tano kupitia mashine mbili, na bwawa lake lina uwezo wa kuhifadhi meta za ujazo milioni 1.14 za maji.
Hapa, utalii wa kupiga picha, kuogelea na kuendesha mtumbwi huenda sambamba na nishati safi kwa jamii.
Fukwe, Visiwa na Wanyama Pori
Kuelekea wilaya ya Namtumbo na Tunduru, Mto Ruvuma hubadilika kuwa mto wa ndoto kwa watalii.
Hifadhi ya mazingira asilia ya Mwambesi inatoa mandhari ya kipekee ,visiwa vidogo, fukwe nzuri, na safari za mitumbwi.
Hapa, tembo, simba, swala, mamba, na samaki wa aina mbalimbali hutawala kando mwa Mto Ruvuma wakivutia watalii kutoka ndani na nje ya nchi.
Katika Pori la Akiba la Liparamba wilayani Nyasa, maporomoko ya Nakatuta ni kivutio kingine. Wageni huja kuvua samaki, kupiga picha, na kupanda miamba ya asili iliyobeba historia ya miaka mingi.
Historia Iliyogubikwa na Maajabu
Mto Ruvuma haujaishia kwenye uzuri wa kiasili pekee; ni shahidi wa harakati za uhuru. Katika eneo la Mwambesi, maji haya yalitumika katika Vita ya Majimaji (1905–1907), na maporomoko ya Sunda yalitumika kama “darubini ya vita ya porini” ya Golira War iliyopiganwa Msumbiji.
Katika eneo hili, ndege mdogo zaidi duniani pantiole huogelea na kuwinda samaki hai, tukio adimu la kihistoria na kibaiolojia.
Mto Ruvuma Unaounganisha Mataifa
Safari ya Mto Ruvuma inaishia katika daraja la Umoja, mpakani mwa Tanzania na Msumbiji, wilayani Nanyumbu. Daraja hilo lenye urefu wa zaidi ya meta 700 linaunganisha mataifa mawili na siyo kwa daraja pekee, bali kwa urithi wa pamoja wa historia, utalii na amani.
“Mto huu siyo tu mpaka wa kijiografia, bali ni mpaka wa kipekee unaounganisha historia ya ukombozi wa Msumbiji kupitia kijiji cha Negomano, ambacho maana yake ni ‘makutano ya mito’,” anasema Afisa Mahusiano wa Kituo cha Uhamiaji Mtambaswala, Mwamba Lihami.
Bahari ya Hindi: Hitimisho la Safari
Mwisho wa safari ya Mto Ruvuma ni katika Bahari ya Hindi, eneo la Msimbati, Mtwara. Hapa, maji ya mto huingia katika Hifadhi ya Bahari ya Ghuba ya Mnazi na Maingilio ya Mto Ruvuma, hifadhi yenye ukubwa wa kilomita za mraba 650.
Ni eneo lenye utajiri wa viumbe vya majini, mikoko, na mandhari ya kupendeza .
Hakuna shaka Mto Ruvuma si tu kivutio, bali ni chemchemi ya uhai kwa Watanzania na majirani zao wa Msumbiji.
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 S.L.P 74,SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: KERO PIGA 0800110174
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.