Mwenge wa uhuru umeendelea na mbio zake mkoani Ruvuma kwa kupitia miradi kumi yenye thamani ya shilingi bilioni 1.2 katika Halmashauri ya Mji wa Mbinga.
Kiongozi wa mbio za mwenge kitaifa wa uhuru 2025 Ndugu Ismail Ali Ussi amepongeza usimamizi wa miradi ya maendeleo uliofanywa na viongozi kwa kushirikiana na wananchi hali iliyosababisha miradi kuwa na viwango bora.
Moja ya miradi iliyopitiwa na mwenge wa uhuru ni ujenzi wa shule mpya ya sekondari Kata ya Betherehemu ambapo serikali imetenga kiasi cha shilingi milioni 740 kutekeleza mradi huo kupitia program ya uboreshaji elimu ya sekondari (SEQUIP).
Mwenge wa uhuru pia umekagua na kufungua mradi wa maji Mkwaya unaokadiriwa kugharimu Zaidi ya shilingi milioni 375 na unatarajia kuhudumia wananchi 1,853.
Meneja wa RUWASA wilaya ya Mbinga Mhandisi Yona Ndomba amesema hadi sasa utekelezaji wa mradi huo umefikia asilimia 100 na tayari kaya 13 zimeunganishwa na huduma ya maji majumbani.
Mwenge wa uhuru ukiwa katika Halmashauri ya mji wa Mbinga umekagua mradi wa huduma za afya zinazotolewa na jengo la OPD katika zahanati ya Mtakatifu Gabriel inayomilikiwa na Jimbo katoliki la Mbinga.
Askofu wa Jimbo la Mbinga Mhashamu John Ndimbo amesema ujenzi wa jengo la wagonjwa wa nje OPD ni sehemu tu ya ujenzi wa mradi mzima wa kituo cha afya tarajiwa cha St.Gabriel Jimbo katoliki la Mbinga.
Amesema mradi wa OPD umegharimu Zaidi ya shilingi milioni 100 ukiwa ni msaada kutoka kwa wafadhili na majitoleo ya waumini.
Mwenge wa uhuru ukiwa katika Halmashauri ya Mji wa Mbinga pia umekagua mradi wa shamba la miti linalomilikiwa na Ndugu Lukas Nchimbi Mkazi wa kijiji cha Utiri .
Shamba hilo lina ukubwa la hekari 10.4 likiwa na jumla ya miti ya kupanda 4,600 na kwamba mradi huo una thamani ya shilingi milioni 32.
Mwenge wa uhuru pia ukiwa mjini Mbinga umetembelea na kukagua kikundi cha UMOJA kinachofanya shughuli za ufundi seremala na kuchakata mazao ya misitu ili kuongeza kipato cha wanakikundi ambapo hadi sasa mradi umegharimu shilingi milioni 33.
Akizungumza baada ya kukamilisha kupitia miradi hiyo Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru kitaifa 2025 Ndugu Ismail Ali Ussi ameupongeza uongozi wa Wilaya,Halmashauri na wananchi kwa usimamiaji mzuri wa miradi ukiwemo mradi mpya wa shule ya sekondari Kata ya Betherehemu ambayo itawapunguzia watoto umbali wa kwenda mbali kufuata shule ya sekondari.
Amepongeza ujenzi wa shule hiyo ambayo amesema ni bora na ina viwango vinavyolingana na thamani ya fedha
“Mimi binafsi wakati naingia katika shule hii nilikuwa najiuliza hii ni shule au hoteli,mkuu wa wilaya aliniambia hii ni shule,shule kama hii tulikuwa tumezoea kuiona katika maeneo maalum kama Dar es salaam,tuna kila sababu ya kumpongeza Rais kwa kutoa fedha za ujenzi wa shule hii’’,alisisitiza Ussi.
Kiongozi huyo wa mwenge wa uhuru ameendelea kuwakumbusha wananchi kuwa mwaka huu ni mwaka wa uchaguzi hivyo wote waliojiandikisha wasisite kujitokeza kuwachagua viongozi katika uchaguzi Mkuu utakaofanyika Oktoba mwaka huu.
Mwenge wa Uhuru upo mkoani Ruvuma tangu Mei 9 hadi Mei 17 mwaka huu utakapokabidhiwa katika Mkoa wa Mtwara
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 S.L.P 74,SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: KERO PIGA 0800110174
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.