MWENGE wa uhuru 2025 umepitia na kuridhishwa na utekelezaji wa miradi tisa yenye thamani ya shilingi bilioni 82 katika wilaya ya Nyasa mkoani Ruvuma.
Mkuu wa Wilaya ya Nyasa Mheshimiwa Peres Magiri amesema kati ya miradi hiyo,Mwenge wa Uhuru umekagua miradi mitatu,umeweka jiwe la msingi mradi mmoja na kuzindua miradi mitatu na miradi miwili kugawa vyandarua
Akitoa taarifa kwa Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa 2025,Meneja wa RUWASA Wilaya ya Nyasa Mhandisi Masoud Samila amesema utekelezaji wa mradi huo umefikia asilimia 40 na kwamba wananchi 4,490 watapata maji safi kupitia mradi huo.
Mwenge wa Uhuru pia umezindua mradi wa mtambo za kufua hewa tiba (Oxygen plant) ambapo kiasi cha shilingi milioni 480 zimetumika kujenga miundombinu ya gesi na ununuzi wa mtambo wa kuchakata hewa tiba.
Mradi huu umekuwa na faida kubwa katika utoaji wa huduma za afya hospitalini ikiwemo kusogeza huduma jirani na kupunguza gharama za kununua huduma.
Mwenge wa uhuru umekagua shughuli za kikundi cha wajasiriamali vijana katika kijiji cha Ruhekei Kata ya Kilosa ambapo kikundi hicho kimefanikiwa kupata mkopo wa shilingi milioni 16.5 .
Akitoa taarifa ya kikundi hicho Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Nyasa Khalid Khalif amesema mkopo huo unatokana na fedha za asilimia kumi ya mapato ya ndani ya Halmashauri hiyo.
Mradi mwingine uliozinduliwa na Mwenge wa uhuru ni ujenzi wa vyumba vitatu vya madarasa katika shule ya sekondari Limbo ambapo serikali ilitenga shilingi milioni 72 kutekeleza mradi huo.
Kukamilika kwa mradi huo kumeboresha mazingira ya kufundishia na kujifunzia wanafunzi hivyo kupunguza mlundikano wa wanafunzi darasani.
Mwenge wa Uhuru pia umetembelea na kukagua mradi wa kimkakati wa ujenzi wa bandari na barabara ya kuingia bandari ya Mbambabay kwa kiwango cha zege.
Meneja wa Bandari katika ziwa Nyasa Manga Gassaya amesema serikali imetenga Zaidi ya shilingi bilioni 82 kutekeleza mradi wa bandari ya Mbambabay na kwamba mradi huo unatarajia kukamilika Januari,2026.
Mwenge wa Uhuru ukiwa wilayani Nyasa pia umepitia miradi ya wapinga rushwa katika sekondari ya Kingerekiti na utekelezaji wa shughuli za lishe ambapo wilaya hiyo imetumia Zaidi ya shilingi milioni 33 sawa na asilimia 100 kugharamia afua za lishe kwa watoto 32,574.
Mwenge wa uhuru umekagua mradi wa kugawa vyandarua vyenye thamani ya shilingi 500,000 ambapo katika wilaya ya Nyasa mwaka 2024 jumla ya watu 14,412 waliugua ugonjwa wa malaria.
Wilaya ya Nyasa inaendelea na mapambano dhini ya malaria kwa kugawa vyandarua kwa watoto chini ya miaka mitano jumla ya wajawazito 7,325 na watoto 9,114 walipatiwa vyandarua mwaka 2024.
Akizungumza baada ya kukagua miradi hiyo ukiwemo mradi mkubwa wa kimkakati wa ujenzi bandari ya Mbambabay,Kiongozi wa mbio za Mwenge wa uhuru 2025, Ismail Ali Ussi Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan ametoa mabilioni ya fedha kuhakikisha mradi wa bandari ya kisasa unakamilika.
“Leo hii tumekuja kujionea bandari ya kisasa inayokwenda kutuunganisha na nchi jirani.serikali imefanya uwekezaji mkubwa wa bandari,mradi ambao unatarajia kukamilika mapema mwaka 2026”,alisema.
Katika hatua nyingine Kiongozi huyo wa mwenge wa Uhuru amewakumbusha wananchi kujitokeza kwa wingi kwenye uchaguzi Mkuu Oktoba mwaka huu kwenda kupiga kura.
Amesema Mwenge wa uhuru ni chombo kinachomwakilisha Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan na kwamba unapouona mwenge wa Uhuru utambue kuwa Rais yupo katika eneo hili.
Mwenge wa uhuru upo mkoani Ruvuma kuanzia Mei tisa hadi Mei 17 utakapokabidhiwa mkoani Mtwara.
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 S.L.P 74,SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: KERO PIGA 0800110174
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.