Na Albano Midelo
ENEO la Masonya lililopo katika Halmashauri ya Wilaya ya Tunduru mkoani Ruvuma lina utajiri wa utalii wa malikale na utambulisho wa Taifa, ingawa bado halifahamiki na wengi.
Eneo hilo lenye ukubwa wa ekari 100 lina vivutio adimu vya utalii wa malikale ikiwemo nyumba yenye namba A 10 ambayo walikuwa wanafikia na kuishi Marais Hayati Julius Nyerere wa Tanzania na Hayati Samaro Machel wa Msumbiji kuanzia 1966 hadi mwaka 1975 wakati wa harakati za ukombozi Kusini mwa Afrika.
Mhifadhi wa Makumbusho ya Taifa ya Majimaji Bartazar Nyamusya anasema viongozi hao pia wakiwa katika nyumba hiyo, walitumia jengo dogo maalum lililopo jirani ya nyumba hiyo kama chumba cha mawasiliano yote na nchi zilizokuwa katika harakati za ukombozi kusini mwa Afrika.
Moja ya mambo yanayovutia katika eneo la Masonya ni kwamba Rais wa sasa wa Msumbiji Mheshimiwa Filipe Nyusi akiwa na wazazi wake katika harakati za ukombozi wa nchi hiyo,alifika Masonya mwaka 1970 akiwa na miaka nane na kusoma katika shule ya msingi FRELIMO iliyokuwa katika Kata ya Masonya.
Mhifadhi wa Makumbusho ya Taifa ya Majimaji anasema mwaka 1966 Tanzania iliwapokea wapigania uhuru wa Msumbiji na kuwakabidhi eneo la Masonya.
Hata hivyo anasema eneo hili limebaki kama eneo la makumbusho ambapo ametaja urithi unaopatikana katika eneo hilo kuwa ni nyumba mbili za viongozi wa kitaifa hayati Samora Machel Rais wa kwanza wa Msumbiji na Nyumba aliyokuwa anafikia baba wa Taifa hayati Mwl.Julius Nyerere.
Anautaja urithi mwingine kuwa ni ukumbi wa semina aliokuwa anatumia Samora Machel kutoa mafunzo mbalimbali na majengo 11 ambayo kwa sasa ni madarasa ya wanafunzi wa sekondari ya wasichana Masonya.
Maeneo mengine ya urithi ni mahandaki yaliyotumiwa na wapigania uhuru wa Msumbiji,eneo la bendera ya FRELIMO na eneo la mnara ulipofanyika mkutano wa wanawake wa Msumbiji tarehe 17/3/1973 .
Mwaka 1975 baada ya nchi ya Msumbiji kupata uhuru wapigania uhuru hao walirudi katika nchi yao na kuanzia mwaka 1990 Halmashauri ya Tunduru iliamua kuanzisha shule ya sekondari ya wasichana Masonya yenye wanafunzi wa kidato cha kwanza hadi cha sita.
Eneo la malikale la Masonya linatakiwa kuendelezwa kwa sababu linaweza kutoa mchango mkubwa katika nyanja za utalii, uchumi, elimu na utafiti.
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 S.L.P 74,SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: 0252602256
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.