Jeshi la Polisi Mkoa wa Ruvuma Kitengo cha Usalama Barabarani limefanya operesheni ya kushtukiza ya ukaguzi wa vyombo vya moto vya kusafirisha abiria na malori. Ukaguzi huo umebaini makosa kadhaa, yakiwemo magari mabovu, uchanganyaji wa mizigo na abiria, na madereva kuendesha magari huku leseni zao zikiwa zimeisha muda wa matumizi.
Mkuu wa Kikosi cha Usalama Barabarani Mkoa wa Ruvuma, Issa Milanzi, aliongoza operesheni hiyo akiwa ameambatana na waandishi wa habari. Ukaguzi ulifanyika katika stendi ya mabasi ya Seedfarm na eneo la Msamala.
“Gari haina honi, indiketa hazifanyi kazi, lakini dereva huyu anadiriki kusafirisha abiria. Pia kuna gari haina plate namba halali, badala yake imebadilishwa kinyume cha sheria,” alisema RTO Milanzi wakati wa ukaguzi
RTO Milanzi amewataka madereva wote mkoani Ruvuma kufuata sheria, kanuni, na taratibu za usalama barabarani ili kuepusha ajali zinazoweza kuzuilika. “Unapokwenda kinyume na sheria, unaweza kusababisha matatizo ambayo yangepaswa kuepukika kwa kufuata taratibu,” alisisitiza.
Madereva wa mabasi ya shule nao wamekumbushwa kufuata sheria ili kuhakikisha watoto wanafika salama shuleni na kurudi nyumbani bila ajali.
Jeshi la Polisi Kikosi cha Usalama Barabarani limejipanga kuondoa magari yasiyokidhi viwango barabarani na kuhakikisha usalama wa abiria na watumiaji wa barabara.
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 S.L.P 74,SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: 0252602256
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.