Na Albano Midelo,Songea
SERIKALI ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan imetoa zaidi ya shilingi bilioni 15 kupitia program ya Uboreshaji Elimu ya Sekondari (SEQUIP) kujenga sekondari mpya za mfano 21 mkoani Ruvuma.
Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Kanali Laban Thomas anasema kati ya sekondari hizo,katika awamu ya kwanza ya SEQUIP zimejengwa sekondari 11 zilizogharamu shilingi bilioni 7.7 ikiwemo sekondari moja ya wasichana ya Kitaifa iliyojengwa wilayani Namtumbo kwa gharama ya shilingi bilioni nne.
Kulingana na Mkuu wa Mkoa katika awamu ya pili ya SEUIP serikali imetoa zaidi ya shilingi bilioni 6.44 kujenga sekondari mpya za sekondari 10 katika Halmashauri zote nane za Mkoa wa Ruvuma.
Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Kanali Laban Thomas anasisitiza kuwa Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan ametoa fedha hizo ili kujenga shule mpya za sekondari za kata katika kata zisizo na shule na kata zenye wanafunzi wengi zaidi ukilinganisha na miundombinu ya shule zilizopo.
Afisa Elimu wa Mkoa wa Ruvuma Mwl.Edith Mpinzile anasema katika Halmashauri ya Tunduru zimejengwa shule tano za sekondari kupitia mradi wa SEQUIP na kwamba katika Halmashauri ya Namtumbo zimejengwa shule za sekondari tatu ikiwemo shule ya kitaifa ya wasichana ya Mkoa wa Ruvuma.
Kulingana na Afisa Elimu huyo katika Halmashauri ya Manispaa ya Songea zimejengwa sekondari mbili,Halmashauri ya Madaba sekondari mbili, Halmashauri ya Songea sekondari mbili, Halmashauri ya Wilaya ya Mbinga sekondari mbili,Halmashauri ya Mji wa Mbinga sekondari mbili na Halmashauri ya Nyasa sekondari mbili.
“Mradi wa SEQUIP umewezesha kila shule ya sekondari kuwa na jengo la utawala,vyumba vya madarasa nane, vyoo matundu 12,mfumo wa maji, maabara tatu,maktaba tatu,kichomea taka na jengo la TEHAMA ”,anasema.
Anasema sekondari 20 zilizojengwa mkoani Ruvuma kupitia SEQUIP awamu ya kwanza na ya pili zimekamilika na kuanza kuchukua wanafunzi ambapo sekondari moja inaendelea kujengwa katika Kata ya Tanga Manispaa ya Songea.
Wanafunzi walioanza masomo katika sekondari hizo wanaipongeza serikali kwa kuwajengea sekondari hizo ambazo zimemaliza changamoto ya wanafunzi kusafiri umbali mrefu kufuata sekondari.
Juma Issa na Khadija Kassim ni wanafunzi wa sekondari mpya Kata ya Tinginya wilayani Tunduru wanasema kabla ya ujenzi wa sekondari hii,wanafunzi waliofaulu katika Kata hiyo walikuwa wanakwenda kusoma katika sekondari ya Nakapanya ambayo ipo umbali wa kilometa 40.
“Kutokana na umbali huo wanafunzi wengi waliacha shule,utoro ulikuwa mwingi na Watoto wa kike walipata mimba baada ya kukumbwa na vishawishi vingi’’,alisema Khadija Kassim.
Mariam Ismail ni Mwananchi kutoka Kijiji cha Tinginya wanasema kabla ya sekondari hiyo wazazi walipata gharama kubwa kwa Watoto wao ikiwemo nauli ya kusafiri Kwenda sekondari ya Nakapanya ambapo baadhi ya wazazi walishindwa kumudu ambapo hivi sasa wanamshukuru Rais kwa kuwajengea sekondari hiyo.
Mkuu wa sekondari ya Tinginya Romatus Ndoa anasema walipokea kiasi cha shilingi milioni 560 ambazo zimetumika kujenga jengo la utawala,madarasa manane,vyumba vitatu vya maabara,jengo la TEHAMA,kichomea taka,minara miwili ya maji na vyoo matundu 12,
Anabainisha kuwa wanafunzi wameanza masomo tangu Januari mwaka huu ambapo sekondari hiyo ya kisasa na mazingira ya kuvutia imeondoa kabisa changamoto ya wanafunzi wa Kata ya Tinginya kusafiri umbali mrefu.
Teresia Ng’ombo ni Kaimu Mkuu wa shule ya sekondari Tuwemacho wilayani Tunduru ambaye anasema wamepokea wanafunzi 70 kati ya 87 waliopangiwa kuanza kidato cha kwanza katika sekondari hiyo.
Zamda Yusufu na Siyawezi Libadi ni wanafunzi wa kidato cha kwanza katika sekondari ya Tuwemacho wanasema ujenzi wa sekondari hiyo umemaliza tatizo la wanafunzi kusafiri kilometa 45 hadi sekondari ya Namasakata kufuata shule.
Kwa upande wake Kaimu Mkuu wa shule ya sekondari Mputa wilayani Namtumbo Filbert Mbunda anasema sekondari hiyo imepokea wanafunzi wa kidato cha kwanza wapatao 157 kati yao waliomaliza darasa la saba mwaka 2023 ni 135 na waliomaliza darasa la saba mwaka 2022 ni 22.
Anasema kabla ya kuanza sekondari hiyo wanafunzi wote waliokuwa wanafaulu darasa la saba walipelekwa sekondari ya Mbunga iliyopo Kata ya Kitanda ambapo walikuwa wanatembea umbali wa kilometa 30 kila siku hali iliyosababisha wanafunzi wengi kuacha shule.
Naye Mkuu wa shule ya sekondari ya Lilondo Subira Mapunda anasema baada ya shule hiyo kukamilika wamepokea wanafunzi wa kidato cha kwanza ambao walikuwa wanasafiri umbali wa kilometa 20 hadi sekondari ya Wino ambapo hivi sasa wanafunzi wanafurahia mazingira mazuri ya kujifunzia.
Ado Kawonga ni Kaimu Mkuu wa sekondari ya Mtopesi iliyojengwa katika Kijiji cha Lugagara Halmashauri ya Wilaya ya Songea anasema mara baada ya kukamilisha ujenzi wamepokea wanafunzi 71 wa kidato cha kwanza hivyo kumaliza changamoto ya wanafunzi kutembea kilometa 30 kila siku kufuata sekondari ya Kilagano.
Petro Liweli ni Mkuu wa shule ya sekondari ya Dkt.Lawrence Gama iliyopo Kata ya Mkuzo Manispaa ya Songea anasema wamepokea jumla ya wanafunzi wa kidato cha kwanza 200 ambao wameanza masomo mwaka huu .
Serikali kupitia SEQUIP awamu ya pili katika mwaka 2022/2023 imetoa zaidi ya shilingi bilioni 100 kwa ajili ya ujenzi wa sekondari mpya za kata 176 kati ya hizo sekondari kumi zimejengwa mkoani Ruvuma.
Serikali ya Awamu ya Sita imtenga shilingi Trilioni 1.2 kupitia program ya SEQUIP kujenga shule mpya za sekondari 1000 katika nchi nzima zikiwemo sekondari mpya 26 za kitaifa kwa ajili ya wasichana ambazo zinajengwa kwa kipindi cha miaka mitano katika nchi nzima
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 S.L.P 74,SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: 0252602256
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.