ZOEZI la sensa ya mifugo,kilimo na uvuvi linatekelezwa kwa miezi miwili ndani ya Mkoa wa Ruvuma kwa kufanya madodoso katika kaya 1498 .
Meneja wa Takwimu mkoani Ruvuma Mwamtum Athuman Uhenga amesema zoezi hilo ambalo linaendelea katika nchi nzima katika Mkoa wa Ruvuma limeanza Agosti 5 mwaka huu na linaratajia kukamilika Oktoba 3 mwaka huu.
Amesema katika zoezi hilo kutakuwa na madodoso matatu ambayo yatakwenda kuhojiwa katika kaya zilizochaguliwa.
Ameyataja madodoso hayo kuwa ni dodoso la wakulima wakubwa,dodoso la wakulima wadogo na dodoso la jamii ambalo linachukuliwa katika ngazi ya kijiji au mtaa ambao umechaguliwa katika sensa hiyo.
“Taarifa ambazo zinakwenda kukusanywa ni za uzalishaji kwa mwaka wa kilimo wa 2019/2020,taarifa zinazoanzia Oktoba Mosi,2019 hadi Septemba 30,2020’’.alisema.
Hata hivyo Uhenga amesema hadi sasa hakuna changamoto iliyojitokeza ambapo amewashukuru wananchi wa Mkoa wa Ruvuma kwa kutoa ushirikiano mkubwa kwa watalaam wa takwimu wakati wa utekelezaji wa zoezi hilo la kitaifa.
Kwa upande wake Kaimu Katibu Tawala wa Mkoa wa Ruvuma Seligius Ngai akizungumza na wananchi wa kijiji cha Mbingamhalule wilayani Songea baada ya kukagua zoezi la madodoso ,amesema takwimu ni uti wa mgongo wa shughuli za serikali.
Ngai amesema takwimu bora zinahitajika kwa maendeleo bora ambapo amezitaja sifa za takwimu bora kuwa ni zile ambazo zimekusanywa na mamlaka husika,kwa kufuata sheria ya takwimu ya mwaka 2015.
Amesisitiza kuwa ofisi ya Taifa ya Takwimu inahusika moja kwa moja na kukusanya,kuchakata na kutoa taarifa rasmi ambapo amesema zoezi linaloendelea limejikita katika sekta tatu za kiuchumi ambazo ni mifugo,kilimo na uvuvi.
“Katika kilimo tunataka kujua hali ya mazao yetu na changamoto zake,katika mifugo kujua idadi ya mifugo iliyopo,magonjwa ya mifugo na masoko ya mazao ya mifugo’’,alisema.
Ngai amesema mipango yote ya maendeleo inayotekelezwa na serikali,nyuma yake kuna takwimu na kwamba hata Benki ya Dunia ilivyoitangaza Tanzania kuingia kwenye uchumi wa kati nyuma yake kuna takwimu.
Naye Said Ameir Afisa Mawasiliano Ofisi ya Taifa ya Takwimu Makao makuu ametoa rai kwa wananchi kutoa taarifa sahihi ambazo zitatoa takwimu sahihi ambazo zitaleta mpango ambao unawakilisha hali halisi na kutengeneza sera na kupanga mipango mbalimbali ya maendeleo katika sekta ya kilimo,uvuvi na mifugo.
Franki Hyera Mkazi wa kijiji cha Mbingamhalule ameishukuru serikali kwa kuanza kufanya sensa ya mifugo,kilimo na Uvuvi ambapo amesema mpango huo utaleta manufaa makubwa kwa wananchi baada ya kupata takwimu katika kijiji hicho ambacho kinazalisha kwa wingi mazao ya chakula.
Zoezi la Sensa ya kilimo,mifugo na uvuvi hapa nchini linafanyika kwa mara ya tano mwaka huu.Zoezi hili lilianza kufanyika kwa mara ya kwanza hapa nchini mwaka 1972,na kufanyika tena mwaka 1994,2003 na mwaka 2008.
Imeandikwa na Albano Midelo
Afisa Habari Mkoa wa Ruvuma
Agosti 30,2020
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 S.L.P 74,SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: 0252602256
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.