Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan imetoa shilingi bilioni 9.345 kujenga vituo vya afya 14 mkoani Ruvuma.
Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Kanali Ahmed Abbas Ahmed amesema fedha hizo zimetolewa kupitia fedha za mapato ya ndani, Tozo, Serikali Kuu na Wahisani.
Amesema vituo vyote vinajumuisha ujenzi wa majengo ya huduma ya mama na mtoto pamoja na majengo ya upasuaji.
Ameongeza kuwa serikali pia imejenga majengo manne ya huduma za dharura (EMD) Kwa gharama ya Zaidi ya Shilingi bilioni 1.5.
Ameyataja majengo ya EMD kuwa yamejengwa katika hospitali ya Rufaa ya Mkoa,Songea,Hospitali ya wilaya ya Tunduru,Madaba na Nyasa na kwamba serikali imejenga jengo moja
la wagonjwa mahututi kwa gharama ya shilingi milioni 250 katika hospitali ya Halmashauri ya wilaya ya Mbinga.
Ameongeza kuwa serikali pia imetoa Zaidi ya shilingi milioni 152 kwa ajili ya ukarabati wa jengo la wagonjwa mahututi (ICU) katika hospitali ya Rufaa ya Mkoa,Songea.
Kwa mujibu wa Mkuu wa Mkoa,Serikali pia imetoa Zaidi ya shilingi bilioni 5.1 kwa ajili ya kuendeleza ujenzi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa,Songea katika Kata ya Mwengemshindo Manispaa ya Songea.
Amesema Mkoa wa Ruvuma unaendelea na ukamilishaji wa Ujenzi wa zahanati 21 kwenye Halmashauri saba kwa gharama ya shilingi bilioni 1.05 na ukamilishaji wa Ujenzi wa Hospitali tano za Wilaya kwa gharama ya Shilingi Bilioni 3.4.
Akizungumzia hali ya upatikanaji wa dawa, vifaa, vifaa tiba na vitendanishi katika vituo vya kutolea huduma za afya mkoani Ruvuma,Kanali Abbas amesema hali imeendelea kuimarika, kwa kuwa upatikanaji umeongezeka kutoka asilimia 93 mwaka 2021 hadi kufikia asilimia 96 mwaka 2023.
Amesema Mkoa umepokea mashine ya CT scan na digital X-ray kwa ajili ya hospitali ya Rufaa ya Mkoa na mashine ya X-Ray kwa ajili ya hospitali ya Halmashauri ya Wilaya ya Madaba ili kuboresha huduma za afya kwa wananchi.
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: 0252602256
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.