Hekari moja kuingiza milioni 16
Na Albano Midelo,Songea
UTAFITI uliofanywa na Taasisi ya Kuendeleza Kilimo Nyanda za Juu Kusini (SAGCOT) katika Wilaya ya Songea mkoani Ruvuma kuanzia mwaka 2020 hadi 2024 umebaini kuwa viazi mviringo vimetoa matokeo mazuri katika uzalishaji.
Afisa Kilimo kutoka Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Onesmo Mpuya akizungumza kwenye zoezi la kuzindua uvunaji wa zao la viazi mviringo katika shamba darasa la majaribio Kata ya Tanga Manispaa ya Songea ya Songea, amesema SAGCOT wamefanya utafiti wa kulima viazi mviringo katika vijiji vya Liganga,Mang’ua na Tanga wilayani Songea na zao hilo kuonesha mafanikio makubwa katika uzalishaji.
“Watu wengi wanaamini viazi mviringo vinastawi vizuri mkoani Njombe na hata mimi nilikuwa naamini hivyo,kumbe kama huna utafiti huna haki ya kusema,utafiti wetu wilayani Songea umebaini viazi mviringo vinafanya vizuri sana’’,alisisitiza Mpuya.
Ametoa rai kwa wananchi wa Mkoa wa Ruvuma kuona fursa ya kutengeneza uchumi na kuongeza kipato kupitia zao la viazi mviringo ambapo utafiti umebaini kuwa heka moja ya viazi mviringo inazalisha magunia 200 hivyo kumuingizia mkulima wastani wa shilingi milioni 16.
Amesema Idara ya kilimo Mkoa wa Ruvuma kwa kushirikiana na SAGCOT inahamasisha kilimo cha parachichi katika Mkoa wa Ruvuma ambapo hadi sasa kuna Zaidi ya hekari 500 ambazo zimepandwa parachichi ambazo ambazo huanza kuzaa baada ya miaka mitatu.
Mgeni rasmi kwenye hafla ya uvunaji viazi mviringo,Mstahiki Meya wa Manispaa ya Songea Mheshimiwa Michael Mbano amesema wakulima wa Songea kwa muda mrefu wamekuwa wakitegemea zao moja la mahindi ambapo amesema zao la parachichi na viazi mviringo linakwenda kuleta fursa mpya na tija kwa wakulima.
Mbano amesisitiza kuwa wakati anapata taarifa za uzinduzi uvunaji viazi mviringo hakuamini kama ardhi ya Songea inafaa kwa kilimo cha zao hilo na kwamba wananchi wengi wa Songea hawana taarifa kama viazi mviringo vinaweza kustawi na kuwaongezea kipato.
Amesema tani 20 za viazi mviringo ambazo zinavunwa kwa hekari moja ni uchumi ambao kila mwananchi wa Mkoa wa Ruvuma anatamani kupata ambapo pia ametoa rai kwa wananchi wa Songea kulima zao la parachichi ambalo pia linatoa kipato kikubwa
Amesema utafiti umebaini mti mmoja wa parachichi kwa mwaka unaweza kumuingia mkulima kati ya shilingi 500,000 hadi 800,000 hivyo ametoa rai kwa wananchi wa Manispaa ya Songea kupanda miti ya matunda kama parachichi na viazi mviringo ili kukuza uchumi wao.
Naye Mwenyekiti wa Chama cha Wakulima cha LUSITU AGRI BUSSINESS ambaye pia ni Mkulima Mwezeshaji Beno Mgaya ameitaja Taasisi ya Kuendeleza Kilimo Nyanda za Juu Kusini (SAGCOT) imedhamiria kutoa mafunzo ya kilimo biashara ili wakulima waweze kujitambua kwa kuhamasisha kilimo cha parachichi na viazi mviringo katika Mkoa wa Ruvuma.
Amesema utafiti walioufanya katika wilaya ya Songea kuhusu zao la viazi mviringo kwa kutumia mbegu za aina mbili kutoka nchini Uholanzi zimetoa matokeo mazuri na kwamba hapa nchini hivi sasa kuna aina 16 za mbegu za viazi mviringo.
Mgaya amelitaja lengo la kuanzisha kilimo cha viazi mviringo ni kumwezesha mkulima kupata kipato wakati anasubiri zao la parachichi ambalo huchukua miaka mitatu hadi kuanza kuzaa mkoani Ruvuma.
Amesema SAGCOT imedhamiria kuwa na mashamba darasa katika zao la viazi mviringo katika maeneo ya Shule ya Tanga, Liganga,Litapwasi,Namatuhi na Peramiho wilayani Songea na kwamba mashamba darasa yote yapo katika mfumo wa umwagiliaji.
Hata hivyo amesema wakulima wa viazi mviringo mkoani Ruvuma wataweza kuzalisha kwa kutumia umwagiliaji hivyo kuzalisha mwaka mzima na kumwezesha mkulima kupata kipato kizuri Zaidi.
Mwenyekiti huyo anamshukuru Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan kwa kuiamini SAGCOT ili iweze kufanya kazi Tanzania nzima ambapo hadi sasa imeenea katika mikoa tisa.
Kandidus Komba Mkulima Mwamasishaji kutoka Kijiji cha Liganga wilayani Songea, ameipongeza SAGCOT kwa kusimamia mradi huo kwa zao la parachichi ambapo wakulima wa vijiji vya Liganga, Peramiho,Litapwasi,Ndongosi,Lipokela, na Mang’ua,Mtakanini na Geraza la Kitai ,wamenufaika na mradi huo.
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: 0252602256
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.