WAKULIMA wa zao la mbaazi wa Wilaya ya Tunduru mkoa wa Ruvuma, wameuza jumla ya kilo 2,478,000 katika mnada wa kwanza uliofanyika katika Chama cha msingi cha Ushirika Chichilimbe kata ya Mbesa.
Meneja Mkuu wa Chama Kikuu cha Ushirika Tunduru TAMCU Marcelino Mrope amesema,mbaazi hizo zimeuzwa kupitia mfumo wa stakabadhi ghalani kwenye vyama vya msingi vya ushirika ambapo bei wastani ni Sh.1,986 kwa kilo moja.
Mrope amesema,Chama kikuu cha Ushirika katika msimu wa masoko 2024/2025 kitaendelea kuuza mbaazi kwa mfumo wa stakabadhi ghalani, na ununuzi hautakuwa kama hapo awali ambapo wanunuzi walikuwa wanaweka barua katika masanduku siku moja kabla ya mnada.
Kwa mujibu wa Mrope,ununuzi wa mbaazi na mazao yote yaliyoingizwa kwenye mfumo wa stakabadhi ghalani katika msimu wa mwaka huu, uendeshaji wa masoko yake utasimamiwa na Soko la bidhaa Tanzania(TMX)na minada yote itaendeshwa kidijitali.
Ametaja makisio ya uzalishaji wa zao la mbaazi yaliyofanywa na Chama hicho kupitia vyama vya msingi vya Ushirika(AMCOS) msimu wa kilimo 2024/2025 ni kuzalisha kilo 7,050,000.0 ambazo ni ongezeko la kilo 1,991,194 za msimu uliopita.
Katika msimu 2023/2024 Chama kikuu kiliendesha minada mitano ambapo jumla ya kilo 5,058,806.0 za mbaazi zenye thamani ya Sh.bilioni 10,162,065,952.00 ziliuzwa.
Diwani wa kata ya Mbesa Mheshimiwa Daniel Mlanda amesema,wakulima wa kata hiyo wanaongoza kwa uzalishaji wa mbaazi katika wilaya ya Tunduru kwa miaka mitatu mfululizo.
Amewaomba wanunuzi kuendelea kununua zao hilo kwa bei kubwa hata katika minada mingine inayofuata ili kuwahamasisha wakulima kuendelea na uzalishaji katika msimu wa kilimo 2025/2026.
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 S.L.P 74,SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: 0252602256
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.