Mkuu wa Wilaya ya Mbinga Mhe. Cosmas Nshenye amewataka wananchi kuwa watulivu na wavumilivu wakati wanasuburi hatima ya mgogoro wa ardhi eneo la Ndika unaohusisha baadhi ya wananchi wa Wilaya ya Mbinga wanaoendelea na shughuli za kilimo kwenye eneo hilo lililopo Wilayani Nyasa ambalo limepandwa miti.
Katika mkutano wa hadhara uliofanyika kwenye kijiji cha Mkuwani kati ya Mkuu huyo wa Wilaya ya Mbinga na wananchi wa vijiji vya Mkuwani na Mkuka uliofanyika leo aprili 30, Mhe. Nshenye pia ameonya wananchi kujiepusha na vitendo vya kihalifu na kutii sheria huku akiwataka kuwa watulivu hadi hapo mgogoro huo utakapopatiwa ufumbuzi na Waziri wa Ardhi.
Mhe. Nshenye ametoa wito kwa wananchi kufuata taratibu zilizopo pale inapotokea kutoridhishwa na maamuzi yoyote na kwamba sheria imewapa uhuru wa kupeleka malalamiko yao ngazi za juu huku akiwapongeza kwa hatua waliyochukua ya kuwasilisha malalamiko yao kwa Waziri mwenye dhamana na masuala ya ardhi.
Wakizungumza mbele ya Mkuu huyo wa Wilaya, baadhi ya wananchi wamelalamikia kunyanyaswa, kukamatwa na kutozwa faini wanapotembelea mazao yao ya chakula kwenye mashamba yaliyopo eneo la Ndika ambako wamekua wakifanya shughuli za kilimo kwa miaka mingi kabla ya uongozi wa Wilaya ya Nyasa kuanzisha mradi wa kilimo cha miti kwenye eneo hilo ikiwa ni mkakati wa Wilaya hiyo kuhifadhi mazingira ya eneo hilo lililopo kandokando ya Ziwa Nyasa.
Mgororo huo umefikishwa kwa Waziri wa Ardhi na baadhi ya wananchi kutoka kata za Kipapa na Maguu wanaoendelea na shughuli za kilimo kwenye eneo hilo la Ndika wakilalamikia kutoshirikishwa kwenye mchakato wa kubadilisha matumizi ya ardhi hiyo kwa kupanda miti na kwamba hawakubaliani na mpango huo kwa kuwa hawana maeneo mengine ya kulima mazao ya chakula.
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Mbinga, Juma Mnwele akizungumza kwenye mkutano huo amewahakikishia wananchi wa vijiji hivyo kuwa viongozi wa Halmashauri na Wilaya wamekua na nia ya dhati ya kushughulikia mgogoro huo na kwamba jitihada viongozi hao wamekua wakifanya kila jitihada kutafuta suluhu na ufumbuzi wa suala hilo ikiwa ni pamoja na Halmashauri ya Wilaya ya Mbinga kuandaa na kutenga zaidi ya ekari 123 kama maeneo mbadala ya kilimo kwa wananchi wote ambao mashamba yao yemepandwa miti.
Imeandikwa na Salum Said
Afisa Habari Mbinga
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: 0252602256
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.