JUMLA ya watu 68,237 wanaishi na virusi vya UKIMIWI (VVU) Mkoani Ruvuma.
Hayo yamesemwa na Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Kanali Ahmed Abbas Ahmed wakati anazungumza kwenye ufunguzi wa maadhimisho ya siku ya UKIMWI Duniani ambao umefanyika katika uwanja wa Majimaji mjini Songea.
Kanali Abbas amesema kati ya watu hao,wanaume ni 24,959 na wanawake ni 43,238 na kwamba Watoto chini ya umri wa miaka 15 wenye VVU ni 2,382 sawa na asilimia 3.5 na watu wazima wenye umri wa kuanzia miaka 15 ni 65,855 sawa na asilimia 96.5.
Amezitaja Halmashauri zinazoongoza kuwa na idadi kubwa ya watu wenye VVU kuwa ni Manispaa ya Songea yenye watu 18,398,Tunduru watu 9,888 na Halmashauri ya Mbinga watu 9,003.
“Natoa wito kwa waathirika wote kuzingatia tiba na matunzo,ufuasi wa dawa za ARV ni uzima na zinaimarisha afya ya watu wanaoishi na VVU ,hivyo nawaasa wananchi kuacha unyanyapaa na ubaguzi,Mkoa utaendelea kuwajengea mazingira mazuri watu wanaoishi na VVU ili kujiwezesha kiuchumi’’,alisisitiza Kanali Abbas.
Amesema maambukizi ya VVU katika Mkoa wa Ruvuma katika mwaka 2022 hadi 2023 ni asilimia 4.9 na kwamba kiwango hicho kimepungua ukilinganisha na mwaka 2016/2017 ambacho kilikuwa ni asilimia 5.6 .
Hata hivyo amesema kiwango hicho cha maambukizi katika Mkoa wa Ruvuma bado kipo juu zaidi ya kiwango cha kitaifa kwa asilimia 0.5 ambacho ni asilimia 4.4.
Amesema kiwango cha maambukizi mapya ya VVU kimepungua kwa asilimia 28.6 kutoka watu 3.035 mwaka 2017 hadi kufikia watu 2,168 mwaka 2022 ambapo kwa mwaka 2023 watu 1,889 walipata maambukizi mapya ya VVU katika Mkoa wa Ruvuma
Kaulimbiu ya maadhimisho ya UKIMWI kwa mwaka huu ni chagua njia sahihi,tokomeza UKIMWI ambapo kilele cha maadhimisho hayo ni Desemba Mosi ambapo mgeni rasmi anatarajiwa kuwa Makamu wa Rais Dkt.Philip Mpango
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 S.L.P 74,SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: 0252602256
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.