WAZAZI na walezi katika wilaya ya Namtumbo mkoani Ruvuma wametakiwa kuchangamkia fursa ya uwepo wa chuo cha mafunzo ya maliasili kwa Jamii(CBCTC)Likuyu Sekamaganga wilayani humo kwa ajili ya kuwasomesha vijana wao ili waweze kupata ajira ya kuongoza wageni na watalii baada ya kuhitimu masomo yao.
Rai hiyo ilitolewa hivi karibuni na mwakilishi wa katibu mkuu wa wizara ya maliasili na utalii Dkt.Julius Ningu ambaye pia ni mkuu wa wilaya ya Namtumbo wakati alipokuwa akizungumza kwenye mahafali ya pili ya Astashahada ya waongoza watalii 29 chuoni hapo.
Ningu alisema kuwa kutokana na jitihada za Rais Samia Suluhu Hassan kuifungua Tanzania katika masuala ya utalii,wazazi wanapaswa kukitumia chuo hicho kwa ajili ya kusomesha vijana wao ili hapo baadae waweze kujiajiri na kupunguza wimbi la kuzagaa ovyo mitaani bila kazi.
Akizungumza katika mahafali hayo,Ningu amewataka wahitimu hao kujenga utamaduni wa kuwa na tabia ukarimu,uadilifu na uaminifu pindi watakapokuwa wanawaongoza wageni na watalii wanakuja mkoani Ruvuma na Nchini kwa ujumla kwa lengo la kutembelea vivutio mbalimbali.
Aidha amewahasa wahitimu hao kuwa na moyo wa uzalendo katika kutunza maliasili za taifa ambazo zimekuwa zikitoweka na kuharibiwa ovyo na majangili pamoja na watu wanaoendesha shughuli za kibinadamu kwenye hifadhi za wanyama pori.
Naye mwakilishi wa mkurugenzi wa Idara ya wanyamapori Nassoro Wawa ambaye pia ni Afisa wanyamapori mkuu alisema kuwa kuongezeka kwa idadi ya watu kumechangia kwa kiasi kikubwa kufanya shughuli za kibinadamu zikiwemo kujenga,kufanya kilimo na ufugaji kwenye hifadhi za wanyamapori ambapo amewataka wanaoendesha vitendo hivyo kuacha mara moja.
Francisca Malembeka akiongea kwa niaba ya mkurugenzi wa kitengo cha utafiti na mafunzo alisema kuwa mwingiliano wa shughuli za kibinadamu kwenye mapito ya wanyamapori kumechangia uharibifu na kuleta migogoro hivyo amewataka kucha kufanya shughuli hizo na kwamba amewataka wahitimu hao kusaidia kulinda maliasili hizo pamoja na kujisomea vitabu mbalimbali kwa lengo la kuongeza ujuzi na kukaa na wazee kwa ajili ya kujua historia ya mababu wa zamani.
Kwa upande wake mkuu wa chuo hicho Jane Nyau alisema kuwa chuo chake tangu kuanzishwa kwake kimeweza kupata mafanikio mbalimbali ikiwemo kutoa mafunzo kwa wananchi zaidi ya 5000,kuboresha maktaba,kuongeza udahili wa wanafunzi pamoja na kuboresha mabweni.
Nyau alisema kuwa mbali na mafanikio hayo lakini chuo kinakabiliwa na changamoto mbalimbali zikiwemo upungufu wa nyumba za watumishi,uchakavu wa majengo,upungufu wa mabweni,upungufu wa wakufunzi na ukosefu wa mtuza kumbukumbu.
Akisoma taarifa kwa niaba ya wahitimu wenzake,Abdul Mgwasa alisema kuwa elimu waliyoipata wataitumia katika kulinda maliasili za taifa na kuwa mabalozi wazuri wa kukitangaza chuo hicho popote waendapo.
Hata hivyo Mgwasa alisema kuwa katika kipindi chote walichokuwepo chuoni hapo wamekuwa wakikabiliwa na changamoto ya ukosefu wa umeme,mahema,mabweni,ukosefu wa viona mbali pamoja na ajira ya waongoza watalii.
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: 0252602256
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.