KUELEKEA tamasha kubwa la kitaifa la utalii wa kiutamaduni ambalo linatakiwa kufanyika mkoani Ruvuma kuanzia Julai 20 hadi 27 mwaka huu,ni vema kufahamu zao jipya la utalii ambalo limekuwa linafanyika katika nchi zinazoendelea na sasa linafanyika mkoani Ruvuma.
Zao hilo la utalii hapa nchini ambalo kwa mara ya kwanza limefanyika mkoani Ruvuma ni utalii wa kuelea na mitumbwi katika Mto Ruvuma wenye urefu wa Zaidi ya kilometa 800.
Mwaka huu watalii wengine wamefanya utalii wa kuelea na mitumbwi katika Mto Ruvuma,kupiga kasia umbali wa Kilometa 70 kutoka Mpelo wilayani Mbinga hadi katika Pori la Akiba la Liparamba wilayani Nyasa.
Wageni hao wakiwa wanateleza na mitumbwi katika mto huo walishuhudia mandhari za kuvutia na Wanyama mbalimbali wakiwemo mamba,tembo na viboko huku macho ya Wanyama hao wakiangalia mitumbwi ya wageni hao.
Agosti 2019 Mkoa wa Ruvuma kwa mara ya kwanza ulipokea watalii 22 wa kihistoria kutoka barani Ulaya na Marekani ambao wamefanya utalii wa kwanza Tanzania wa kuteleza katika Mto Ruvuma kwa kutumia mitumbwi.
Utalii wa namna hii umekuwa unafanyika katika nchi Afrika ya kusini ambapo kwa Tanzania hii ni mara ya kwanza kupata watalii wanaoteleza kwenye mito, kwa kuwa watalii wanaofika hapa nchini wamekuwa wanatembelea mbuga za wanyama, kupanda milima na maeneo mengine.
Watalii hao walitumia siku kumi kuteleza katika mto Ruvuma umbali wa kilometa 160, kupitia msitu wa Hifadhi wa Taifa wa mazingira asilia wa Mwambesi ambapo kila siku waliteleza kilometa 16 na kuweka kambi katika vijiji vilivyopo kando ya mto huo.
Watalii hao walitumia mitumbwi ya kawaida ya kupiga makasia ambayo imetengenezwa mkoani Arusha na kwamba watalii hao wamemaliza utalii wao kwa usalama.
Watalii waliongozwa na wenyeji ambao wanayajua vizuri maeneo ya mto Ruvuma ambao una miamba, vilima na maporomoko.
Mkoa wa Ruvuma, umeufungua Mto Ruvuma kama chanzo kingine cha utalii Tanzania, cha watalii kufanya utelezi katika mto,huu ni utalii ambao unagharama kubwa na unapatikana katika nchi zilizoendelea duniani.
Wilaya ya Tunduru Septemba 2019 ilipokea watalii wengine 50 kutoka ulaya.Hivi sasa Tunduru imefunguliwa na kupelekwa duniani ambapo Wilaya ya Tunduru ina vivutio vingi vya utalii vikiwemo mbuga za wanyama, ndege na mimea adimu duniani.
Watalii waliotembelea Tunduru wamekabidhiwa nakala ya muongozo wa vivutio vya utalii na uwekezaji katika Mkoa wa Ruvuma ambao ulizinduliwa na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa siku ya kongamano la uwekezaji katika Mkoa wa Ruvuma mwaka 2019.
Safari hiyo ya aina yake ya watalii kutoka Ulaya,licha ya kupata mafanikio makubwa imesaidia kutambua changamoto zikiwemo miundombinu hafifu ya barabara kufikia baadhi ya maeneo kama Msitu wa Taifa wa asili wa Mwambesi.
Watalii hao mara baada ya kumaliza safari yao, wameahidi wanavyorudi katika nchi zao,wanakwenda kutafuta watalii wengine ambao watakuja kuteleza katika Mto Ruvuma.
“Safari yetu ya siku kumi kusafiri katika Mto Ruvuma imethibitisha kuwa Mkoa wa Ruvuma una utajiri wa vivutio vya kipekee vya utalii kama Mto Ruvuma, tunavyorudi nyumbani tunakwenda kupeleka habari hizi kwa wenzetu, hivyo mtarajie kupokea wageni wengi zaidi’’, anasisitiza Dkt. Menagon.
Manyise Mpokigwa ni Meneja Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) Kanda ya Kusini ambao wameratibu ujio wa watalii kutalii katika Mto Ruvuma na Msitu wa Hifadhi wa Taifa wa mazingira asilia Mwambesi wilayani Tunduru, anasema tukio hilo limesaidia kuvitangaza vivutio vilivyopo kusini.
Amesema watalii hao wameongeza pato la Taifa kwa serikali na kwa jamii kwa sababu wakiwa katika vijiji kando kando mwa Mto Ruvuma waliweza kununua bidhaa za wananchi.
Hata hivyo amesema TFS kwa kushirikiana na serikali kuu inaendelea kuboresha miundombinu ya barabara katika misitu hiyo ili watalii wanapoingia kufanya utafiti na utalii waweze kupita kwa urahisi na kuvutia idadi kubwa ya wageni wa ndani na nje ya nchi.
Mto Ruvuma wenye urefu wa kilometa zaidi ya 800 umeanzia Songea mjini kwenye milima ya Matogoro, na kupita katika wilaya zote za Mkoa wa Ruvuma kisha kuendelea katika baadhi ya wilaya za Mkoa wa Mtwara na kumwaga maji yake Bahari ya Hindi.
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: 0252602256
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.