WAZAZI na walezi nchini,wametakiwa kujenga tabia ya kuzungumza na kuwa karibu na watoto wao mara kwa mara,jambo litakalosaidia kupungua kwa vitendo viovu ikiwemo ukiukaji wa maadili ,matumizi ya dawa za kulevya na unyanyasaji wa kijinsia
Wito huo umetolewa na Mhashamu Askofu wa Kanisa Katoliki Jimbo la Tunduru-Masasi Mhasham Filbert Mhasi,katika mahubiri yake kwenye Jubilei ya kutimiza miaka 25 kwa mapadri watatu na miaka 40 ya padri mmoja iliyofanyika katika Kanisa Katoriki Tunduru mjini.
Alisema suala la malezi ya watoto siyo jukumu la viongozi wa kanisa au serikali ,bali kila mmoja katika jamii inawajibu huo ili kupata kizazi salama kitakachoishi kwa kufuata maadili ya Kitanzania na kuzingatia mafundisho ya Mwenyezi Mungu.
Askofu Mhasi ameitaka jamii kukemea mambo mabaya,kuwafundisha watoto wao maadili mema na kuhakikisha wanawapa elimu itakayowasaidia kukabiliana na changamoto za maisha.
“wazazi na walezi tunatakiwa kuzingatia namna gani tunakuwa pamoja na vijana wetu tangu wakiwa watoto, vijana wetu wanahitaji mwongozo wa karibu,tunapowaacha wanatafuta mwongozo sehemu nyingine ikiwemo kwenye mitandao wakifikiri kwamba inawasaidia,kumbe wanaingia kwenye mambo yanayoharibu safari ya maisha yao”alisema.
Aidha,amewaasa watoto na vijana kuwasikiliza wazazi na walezi wao na kuwa karibu nao wakati wote kwa kuwa wazazi wana mambo mema na hawategemei kusikia wala kupata mambo mabaya kutoka kwa watoto wao.
Amewaomba wazazi kupinga kwa nguvu zote mila na desturi zenye madhara zinazochochea na kusababisha kumomonyoka kwa maadili kwa vijana hapa nchini.
Askofu Mhasi,amewataka waumini wa kanisa hilo kuendeleza upendo na mshikamano wao kwa wao na kwa viongozi wao, badala ya kunyoosheana vidole na kushutumiana katika mambo yasiyokuwa na afya kwa kanisa.
Pia,amewataka viongozi wa Dini wakiwemo mapadri na watawa kuendelea kuwa mfano bora na kuhubiri matendo mema ili kuwasaidia waumini wao na jamii kwa ujumla kumjua Mungu wakati wote.
Kwa upande wake Mkuu wa wilaya ya Tunduru Julius Mtatiro,amewapongeza mapadri hao kwa kutimiza miaka 25 na 40 ya utumishi wa kanisa na kueleza kuwa huoni wito mkubwa kuliko yote hapa Duniani.
Mtatiro,ameikumbusha jamii kuacha kupigana majungu na kuchukiana badala yake kuishi kwa upendo na unyenyekevu na kujiepusha na vitendo vinavyokwenda kinyume na maagizo ya Mungu.
Amewakumbusha wana ndoa umuhimu wa kupendana na kuishi kwa amani wakati wote ili kujenga kizazi bora, chenye maadili mema,uaminifu,uadilifu na kinachomjua Mwenyezi Mungu.
Akizungumza kwa niaba ya mapadri wenzake Maiko Tesha alisema,kufika umri wa miaka 25 na 40 katika utumishi ni mapenzi ya Mungu na kuwaomba waumini kuendelea kuwaombea ili waweze kudumu katika majukumu yao.
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 S.L.P 74,SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: 0252602256
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.