Taifa limeingia katika huzuni nzito baada ya kupokea taarifa za kifo cha mwanasiasa mkongwe na shujaa wa mapambano ya uhuru wa Tanganyika, Alhaj Mustafa Mohamed Songambele.
Mzee Songambele, ambaye alitimiza miaka 100 Jumapili iliyopita, amefariki dunia jijini Dar es Salaam, ikiwa ni siku chache tu baada ya kusherehekea karne moja ya maisha yake.
Msiba upo nyumbani kwake Mwananyamala, huku maandalizi ya kuusafirisha mwili kuja Songea kwa ajili ya maziko yakiendelea.
Katika historia ya siasa za Tanzania, jina la Alhaj Songambele haliwezi kufutika. Alikuwa mmoja wa waanzilishi wa Chama cha TANU ,chama kilichoasisi harakati za kudai uhuru akiwa miongoni mwa wanachama wa kwanza 30, na akapewa kadi namba 27.
Baada ya TANU na ASP kuungana na kuunda CCM, aliendelea kuwa mstari wa mbele katika ujenzi wa taifa.
Ni mtu aliyeshuhudia na kushiriki kwa vitendo historia ya ukombozi wa Tanganyika, akiwa bega kwa bega na Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere.
Safari ya uongozi ya Songambele ni sura ya pekee katika historia ya utawala wa nchi.
Aliweka rekodi ya kuwa Mkuu wa Wilaya wa kwanza nchini Tanganyika baada ya uhuru, akiteuliwa kuongoza Wilaya ya Pwani, ambayo leo ni sehemu ya Wilaya ya Ilala.
Hakuishia hapo aliteuliwa kuwa Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, nafasi aliyopewa na Mwalimu Nyerere mwenyewe kutokana na uaminifu, weledi na uzalendo wake usiotetereka.
Alhaj Songambele hakuwa tu kiongozi wa siasa, bali pia mtu wa karibu sana na Mwalimu Nyerere.
Historia inamkumbuka kama mmoja wa wakazi wa Dar es Salaam waliompokea Mwalimu baada ya kuacha kazi ya ualimu ili kujitosa kikamilifu kwenye harakati za kudai uhuru.
Ndiyo aliyemsaidia Mwalimu kupata kiwanja cha kujenga nyumba Magomeni Mikumi nyumba ambayo leo ni kumbukumbu hai ya maisha ya Baba wa Taifa, ikiwa makumbusho rasmi yanayohifadhi historia ya ukombozi wa taifa letu.
Kifo cha Alhaj Songambele si tu pengo kwa familia, bali ni pigo kubwa kwa historia ya Tanzania.. Mzee Songambele amepumzika, lakini historia yake itaendelea kuishi.
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 S.L.P 74,SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: KERO PIGA 0800110174
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.