Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi imezindua mafunzo kwa watendaji ngazi ya mkoa kuhusu Uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura awamu ya pili ambayo itajumuisha Halmashauri tatu za mkoa wa Ruvuma ambazo ni Tunduru DC, Namtumbo DC na Madaba DC.
Uzinduzi huo umefanyika katika ukumbi wa Chandamali mjini Songea mkoani Ruvuma, mgeni rasmi akiwa ni Mjumbe wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi Mhe. Magdalena K. Rwebangira.
Mheshimiwa Rwebangira amewataka watendaji hao hasa wale waliowahi kufanya zoezi kama hilo kutumia uzoefu walionao na mafunzo wanayopatiwa kwa kufanya kazi zao kwa weledi, bidii na moyo wa kujituma ili kufanikisha zoezi hilo.
Ameongeza kuwa wakati wa Uboreshaji wa Daftari mawakala wa vyama vya siasa wataruhusiwa kuwepo katika vituo vya uandikishaji kwa kuwa ni muhimu na itasaidia kuleta uwazi katika zoezi zima na kutambua waombaji wa eneo husika hivyo kupunguza kutokea vurugu zisizo za lazima.
Naye Mratibu wa Uandikishaji Mkoa wa Ruvuma, Salumu Kateula, amebainisha kuwa awamu ya kwanza ya Uboreshaji wa Daftari ambayo ilianza tarehe 12 Januari inatarajia kukamilika Januari 18 ambayo imejumuisha Halmashauri tano katika mkoa linaendelea vizuri, na awamu ya pili ambayo itajumuisha Tunduru DC, Namtumbo DC na Madaba DC itaanza Januari 28 hadi Februari 3, 2025.
Amewasisitiza wananchi wa Halmashauri hizo kutumia muda huo kujitokeza kujiandikisha na kuboresha taarifa zao katika Daftari ili waweze kupata haki yao ya kupiga kura katika uchaguzi ujao.
Kwa upande wake Afisa Muandikishaji Jimbo la Madaba, Sajidu Mohammed, amesema wanaendelea kuwahamasisha wananchi kujitokeza kujiandikisha na kuboresha taarifa zao hasa makundi ya vijana waliotimiza umri wa miaka 18 na watu wenye ulemavu.
Kwa upande mwingine Afisa Muandikishaji Jimbo la Namtumbo, Juma Njelu, amesema anaamini wananchi watajitokeza kwa wingi kujiandikisha ili wapate vitambulisho kwa kuwa vimekuwa vikitumika kwa matumizi mbalimbali ikiwemo mikopo na dhamana.
Awamu ya kwanza ya Uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura mkoani Ruvuma lilianza Januari 12 na linatarajiwa kukamilika Januari 18 katika Halmashauri tano ikiwemo Songea MC, Songea DC, Mbinga TC, Mbinga DC na Nyasa DC na awamu ya pili itaanza Januari 28 na kukamilika Februari 3 mwaka huu.
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 S.L.P 74,SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: 0252602256
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.