Baraza la Madiwani la Halmashauri ya Wilaya ya Tunduru limekutana kujadili rasimu ya makadirio ya bajeti ya mapato na matumizi kwa mwaka wa fedha 2025/26.
Rasimu ya Bajeti hiyo imepitishwa katika Baraza hilo la Madiwani kwa mwaka 2025/26 ni kiasi cha shilingi bilioni 47
Baraza hilo limeongozwa na Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Tunduru Mhe. Hairu Hemed Mussa, ambapo imewasilishwa na Afisa Mipango wa halmashauri hiyo, Bosco Mwingira kwa niaba ya Mkurugenzi mtendaji wa Halmashauri.
Mwingira amesema kuwa bajeti hiyo inalenga kuboresha miundombinu mbalimbali ikiwemo ya afya, elimu, kilimo, na sekta nyingine kwa maendeleo ya wilaya.
Madiwani wa kata ya Mchoteka na Kata ya Ligoma katika baraza hilo wameiomba serikali kushughulikia changamoto zinazowakabili wananchi wa kata zao, ikiwemo ukosefu wa huduma za afya, barabara na maendeleo ya kilimo.
Wamesema hali ya miundombinu katika kata zao inahitaji maboresho makubwa ili kuinua kipato na maisha ya wananchi.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Tunduru Chiza Cypirian Marando, alisema wanaendelea kukamilisha ujenzi wa Zahanati ya Mtangashari, ukarabati wa mabwawa ya samaki, pamoja na kuboresha kilimo cha umwagiliaji ili kuongeza uzalishaji wa mazao.
Aidha, Marando ameeleza kuwa Wilaya ya Tunduru imebarikiwa kuwa na rasilimali za madini aina ya shaba (copper) yanayopatikana katika Kata ya Mbesa ambayo pia yatasaidia kuongeza mapato ya halmashauri.
Mkurugenzi wa Halmashauri ameomba ushirikiano kutoka kwa madiwani na wananchi katika ukusanyaji wa mapato pamoja na kushirikiana katika ujenzi wa madarasa mapya katika Kata ya Ligoma ili kuboresha mazingira ya elimu kwa watoto wa wilaya hiyo.
Kwa upande wake, Makamu wa Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Tunduru ametoa mchango wake akisisitiza uboreshaji wa mapato ya ndani ya halmashauri.
Ameeleza kuwa ukamilishaji wa kilomita 1,206 za barabara unakadiriwa kuchukua takribani miaka nane, hivyo ni muhimu kuweka mkazo katika usimamizi wa fedha na rasilimali zilizopo.
Hata hivyo amesema kuwa bajeti ya fedha kuhusu ukarabati wa barabara kwa upande wao wameiachia Mamlaka ya Wakala wa Barabara Mijini na Vijijini Tarura kushughulikia changamoto hizo.
Katika hitimisho la kikao hicho, madiwani walikubaliana kuwa asilimia 40 ya kiasi cha fedha zilizotengwa zitumike katika uboreshaji wa barabara ndani ya halmashauri.
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 S.L.P 74,SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: 0252602256
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.