Benki ya NMB imekabidhi vifaa vya kuezeka vyenye thamani ya Zaidi ya shilingi milioni 20 kwa shule tatu zilizopo wilayani Nyasa mkoani Ruvuma.
Hafla ya kukabidhi msaada wa vifaa hivyo imefanyika katika shule ya sekondari ya St.Pauls’ iliyopo Kata ya Liuli ambapo mgeni rasmi katika hafla hiyo alikuwa ni Mkuu wa Wilaya ya Nyasa Kanali Thomas Labani.
Akizungumza kabla ya kukabidhi vifaa hivyo kwa Mkuu wa Wilaya,Meneja wa NMB Kanda ya Kusini Janeth Shango amezitaja shule zilizonufaika na msaada huo kuwa ni Shule ya Sekondari St Paul’s Kata ya Liuli, Shule ya Msingi Litoromeo Kata ya Ngumbo na Shule ya Msingi Ngingama Kata ya Linga.
Shango amesema NMB kama wadau wa maendeleo wanao wajibu wa kuunga mkono juhudi za maendeleo zinazofanywa na serikali kwa kusaidia jamii kutatua changamoto mbalimbali zinazowakabili zikiwemo za vifaa vya kuezekea.
“NMB tulipopata Maombi ya kuchangia maendeleo ya elimu katika Wilaya ya Nyasa tuliamua mara moja kuchangia, ili kuwa chachu ya maendeleo katika sekta muhimu ya elimu na kuongeza ari kwa wanafunzi kusoma kwa bidii’’,alisema Shango.
Ameitaja msaada waliochangi katika Shule ya Sekondari St Paul’s kuwa ni bati 200,mbao 725 na Misumari kg 260, katika Shule ya Msingi Litoromeo Bati 100 na nondo 100 na katika Shule ya Msingi Ngingama ni bati 120.
Mgeni rasmi katika hafla hiyo,Mkuu wa Wilaya ya Nyasa Kanali Thomas Laban ameipongeza Benki ya NMB kwa kutoa msaada wa Vifaa hivyo kwa kuwa vitatatua changamoto ya madarasa katika shule hizo.
Hata hivyo Kanali Laban ametoa rai kwa Taasisi nyingine kuiga mfano wa Benki ya NMB wa kusaidia kutatua changamoto mbalimbali katika Sekta ya Elimu ili kuunga Mkono juhudi za Serikali za kuboresha Sekta ya Elimu Nchini.
Mkuu wa Shule ya Sekondari St.Paul’s Liuli Paulo Mwanda ameishukuru Benki ya NMB kwa kutatua changamoto za shule zao na kuahidi vifaa hivyo kuvitumia vizuri kwa malengo yaliyopangwa.
Wanafunzi wa shule hiyo Imanuel Challe Elisha Mpangala na John Mpangala wameipongeza Benki ya NMB kwa kuwatatulia changamoto ya ukosefu wa Bwalo la chakula katika shule yao.
Imeandikwa na Albano Midelo
Nyasa,Julai 7,2022
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 S.L.P 74,SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: 0252602256
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.