SERIKALI ya Awamu ya sita inayoongozwa na Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan imetoa zaidi ya shilingi bilioni 14 kujenga shule mpya za sekondari 11 na vituo vya afya 12 mkoani Ruvuma.
Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Kanali Laban Thomas amesema Mkoa umefanikiwa kujenga shule hizo mpya katika Halmashauri zote nane za Mkoa wa Ruvuma kwa gharama ya shilingi Bilioni 7.7.
“Ujenzi huu unajumuisha shule ya Mkoa ya Wasichana inayojengwa eneo la Migelegele Kata ya Lwinga katika Halmashauri ya Wilaya ya Namtumbo kwa gharama ya shilingi bilioni nne’’,alisema Kanali Thomas.
Hata hivyo amesema Mkoa umefanikiwa kujenga vyumba vya madarasa 792 elimu msingi na sekondari yakijumuisha madawati, viti na meza kwa gharama ya Shilingi Bilioni 14.93
Kwa mujibu wa Kanali Thomas,Mkoa umefanikiwa kujenga mabweni matano ya wanafunzi wa shule za msingi na sekondari kwa gharama ya shilingi Milioni 640 na kwamba Mkoa ulipokea fedha kiasi shilingi milioni 400 kwa ajili ya ukamilishaji wa Maabara 23 za Shule za Sekondari kupitia fedha za Tozo na Serikali Kuu.
Akizungumzia kuhusu sekta ya Afya na Ustawi wa Jamii,Kanali Thomas amesema Mkoa wa Ruvuma umefanikiwa kujenga Vituo vya Afya 12 kupitia fedha za Tozo na Serikali Kuu kwa gharama ya zaidi ya shilingi bilioni 7.8.
Ameongeza kuwa Mkoa umefanikiwa kujenga nyumba tisa za watumishi wa Afya kwa gharama ya shilingi Milioni 856 na kwamba Mkoa umefanikiwa kujenga majengo matatu ya huduma za dharura (EMD) Kwa gharama ya Shilingi Milioni 900.
Kulingana na Kanali Thomas Mkoa wa Ruvuma umefanikiwa kujenga jengo moja la wagonjwa mahututi katika Halmashauri ya Wilaya ya Mbinga kwa gharama ya shilingi milioni 250 na kujenga zahanati 21 kwa gharama ya zaidi ya shilingi bilioni moja.
Hata hivyo amesema Mkoa wa Ruvuma unaendelea na ujenzi wa Hospitali tano za Wilaya ya Nyasa, Halmashauri ya Wilaya ya Mbinga, Halmashauri ya Madaba na Halmashauri ya Songea kwa gharama ya Shilingi bilioni 3.4
Amesema serikali pia inatekeleza mradi wa ujenzi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa awamu ya kwanza katika eneo la Mwengemshindo Manispaa ya Songea kwa gharama ya shilingi bilioni 2.7.
Amesema ujenzi wa hospitali hiyo unahusisha jengo la wagonjwa wa nje (OPD), jengo la mionzi na nyumba ya mtumishi na kuongeza kuwa hali ya upatikanaji wa dawa, vifaa tiba na vitendanishi katika vituo vya kutolea huduma za afya upatikanaji umeongezeka na kufikia asilimia 96.
Imeandikwa na Albano Midelo wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma
Februari 7,2023
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: 0252602256
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.