Wanafunzi wa Shule ya Sekondari ya Wasichana Masonya wilayani Tunduru wamefurahia kuanza kwa ujenzi wa bwalo la chakula, hatua ambayo inaondoa rasmi adha ya kula chakula chini ya miti au ndani ya madarasa.
Furaha yao imeelekezwa kwa Serikali ya awamu ya sita, wakisema kuwa jitihada hizi zinaongeza thamani ya elimu na hadhi ya shule hiyo ya wasichana pekee katika wilaya.
Mwanafunzi Marian Michael, akizungumza kwa niaba ya wenzake, amesema kuwa bwalo hilo ni mkombozi mkubwa hasa ikizingatiwa ongezeko la wanafunzi wa kidato cha tano kwa mwaka wa masomo 2025/2026.
Ameomba mradi huo ukamilishwe kwa wakati ili kutoa huduma mapema.
Mkuu wa shule hiyo, Makrina Ngonyani, amesema ujenzi ulianza Juni kwa kusafisha eneo na tayari kifusi kimeshajazwa katika msingi, huku hatua ya kumwaga zege ikisubiriwa.
Mradi huo unagharimu zaidi ya Shilingi milioni 168 ambapo hadi sasa zaidi ya milioni 102.7 zimetumika.
Ameeleza kuwa shule hiyo imepata mafanikio makubwa katika kipindi cha miaka mitatu kupitia miradi ya ujenzi wa mabweni manne, madarasa, na vyoo kwa zaidi ya Shilingi milioni 775.
Katika ziara yake shuleni hapo, Mkuu wa Wilaya ya Tunduru,Mheshimiwa Denis Masanja, aliwataka mafundi kuongeza kasi ya ujenzi ili bwalo likamilike kabla ya msimu wa mvua. Amewapongeza walimu kwa usimamizi makini wa miradi, akisisitiza umuhimu wa kuendelea kuwa na bidii, nidhamu na upendo kwa wanafunzi huku Serikali ikiendelea kuboresha mazingira ya kazi na maslahi yao.
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 S.L.P 74,SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: KERO PIGA 0800110174
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.