SERIKALI ya Awamu ya sita inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan imeipatia Wilaya ya Namtumbo mkoani Ruvuma kiasi cha shilingi bilioni 1.6 kujenga vyumba 86 vya madarasa.
Mkuu wa Wilaya ya Namtumbo Dkt.Julius Ningu akizungumza katika mradi wa ujenzi wa vyumba vitatu vya madarasa katika shule ya sekondari Nasuli mjini Namtumbo,amesema theluthi moja ya madarasa 86 imefikia hatua ya lenta na ujenzi unaendelea kwa kasi.
“Hadi kufikia Jumamosi ya wiki hii majengo yote ya vyumba vya madarasa 86 katika Wilaya ya Namtumbo yatakuwa yameshafungwa linta na kujiandaa kuezeka wiki inayofuata’’,alisisitiza Dkt.Ningu.
Hata hivyo amesema mifumo mizuri ya usimamizi wa madarasa hayo kwa kuwatumia wenyeviti wa Kamati za Ujenzi wananchi wenyewe kutoka maeneo ya mradi, kumesababisha utekelezaji wa mradi huo kufanyika ndani ya wakati.
Amesema kutokana na maelekezo ya serikali kukamilisha mradi wa madarasa kwa wakati, walijiwekea utaratibu wa kufanya ujenzi kwa awamu kuanzia ujenzi wa msingi,boma,kufunga lenta na kuezeka na kwamba awamu za ujenzi zilikwekwa kwa muda maalum wa siku nne hadi saba katika kila hatua ya ujenzi hali iliyosababisha mradi kwenda kwa kasi kubwa.
Kwa upande wake Mkuu wa shule ya sekondari Nasuli Mwalimu Dafrosa Chilumba ameipongeza serikali kwa mradi wa vyumba vitatu vya madarasa ambao amesema utapunguza uhaba wa vyumba vya madarasa katika shule yake.
Chilumba amesema sekondari hiyo ina jumla ya wanafunzi 1211 wanaosoma katika madarasa 22 na kwamba shule hiyo ilikuwa na upungufu wa vyumba nane hivyo kuongezeka kwa vyumba vitatu vya madarasa kumepunguza kero ya uhaba wa madarasa katika sekondari hiyo yenye kidato cha kwanza hadi cha sita.
Hadija Khamisi ni Mwanafunzi wa kidato cha Tano katika sekondari ya Nasuli,ameipongeza serikali kwa ujenzi wa vyumba vitatu vya madarasa ambavyo amesema vitapunguza msongamano wa wanafunzi madarasani hivyo walimu na wanafunzi kushiriki vema katika kufundisha na kujifunza.
MKOA wa Ruvuma umepokea shilingi bilioni 12.7 sawa na asilimia 2.4 ya shilingi bilioni 635.68 ambazo zimeidhinishwa na TAMISEMI kwa ajili ya uboreshaji wa sekta ya Afya,Elimu na Uwezeshaji wananchi kiuchumi.
Imeandikwa na Albano Midelo
Afisa Habari Mkoa wa Ruvuma
Novemba 22,2021
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 S.L.P 74,SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: 0252602256
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.