Wananchi wa mkoa wa Ruvuma wananufaika na utekelezaji wa miradi ya Maji yenye thamani ya zaidi ya shilingi bilioni 30 zilizotolewa na serikali ya Awamu ya Tano ili kuwaondolea kero ya Maji wananchi.
Hayo yamesemwa na Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Christina Mndeme wakati anakagua mradi wa maji wa Myangayanga Wilaya ya Mbinga ambao serikali inatekeleza kwa gharama ya zaidi y ash.milioni 284.
Mndeme amewaomba wananchi wa Wilaya ya Mbinga kutunza chanzo cha maji cha Miyangayanga chenye uwezo wa kuhudumua watu zaidi ya 12,000 na kinaweza kutoa maji lita laki mbili za maji.
‘’Asante pekee ambayo tunaweza kumpa Rais wetu ni kutunza Mazingira tusifungie kwenye chanzo cha Maji,tusilime,wala kukata miti, Mbinga hatujajaa,tunataka maji haya yanayopatikana katika chanzo hiki yahudumie wakati wa masika na kiangazi bila kupungua’’.alisisitiza Mndeme.
Naye Kaimu Meneja wa RUWASA Wilaya ya Mbinga Mashaka Sinkala amesema Mamlaka hiyo imepanga kufanya ujenzi wa chanzo cha maji,mtandao wa mabomba wa njia kuu hadi kwenye tenki umbali wa kilomita 4.4.
Amesema RUWASA, Wilaya ya Mbinga itaanzisha Jumuiya ya Maji ngazi ya Jamii itakayokuwa na jukumu la kusimamia na kuendesha mradi kwa mujibu wa sheria ya Majina 5 ya 2019 pamoja na kanuni zake za uanzishwaji wa Jumuiya hizo.
Amesema chanzo hicho cha maji ya mserereko kina uwezo wa kuzalisha maji zaidi ya lita za ujazo laki tatu na kinaweza kutosheleza watu zaidi ya 12,000 na kwamba mradi ukikamilika kwa kuanzia utahudumia watu 2,300.
Mradi wa Maji Myangayanga ni miongoni mwa miradi saba inayotekelezwa na RUWASA kwa kushirikiana ya mamlaka ya Maji safi na Usafi wa Mazingira Songea(SOWASA) kwa fedha za mfuko wa Maji kwa utaratibu wa kutumia wataalamu wa ndani katika Wilaya ya Mbinga.
Imeandikwa na Aneti Ndonde
Wa Ofisi ya Habari Mkoa wa Ruvuma
Juni 24,2020
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 S.L.P 74,SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: 0252602256
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.