Wakazi zaidi ya 60,868 wa kata nane katika Halmashauri ya Mji Mbinga, mkoani Ruvuma, wanatarajia kuondokana na changamoto ya ukosefu wa maji safi na salama baada ya Serikali kutenga zaidi ya Shilingi bilioni 4.01 kwa ajili ya kuboresha huduma hiyo muhimu.
Kati ya fedha hizo, Shilingi milioni 755.2 zitatumika kumlipa Mkandarasi Kampuni ya Ngogo Engineering Ltd itakayojenga mradi huo, huku zaidi ya Shilingi bilioni 3.25 zikienda kwa Kampuni ya Simba Pipe Industries Ltd kwa ajili ya kutengeneza na kusafirisha mabomba ya maji kutoka kiwandani hadi Wilaya ya Mbinga.
Akizungumza katika hafla ya utiaji saini mkataba wa mradi huo, Mkurugenzi wa Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Mbinga Mjini (MBIUWASA), Mhandisi Yonas Ndomba, alisema mradi huo utahusisha ujenzi wa vyanzo viwili vya maji vyenye uwezo wa kuzalisha lita 1,613,200 kwa siku, matenki manne yenye ujazo wa lita 525,000 na mtandao wa bomba wa kilometa 57.
Amesema Mradi huu utakapokamilika, huduma ya maji katika kata za Ruhuwiko, Mbinga A, Betherehem, Matarawe, Lusonga, Masumuni, Mbinga Mjini B na Mbambi itapatikana kwa asilimia 97.8.
Hata hivyo amesema hivi sasa, mahitaji ya maji katika Mji wa Mbinga ni lita 5,478,000 kwa siku, wakati uzalishaji halisi ni wastani wa lita 3,797,000, sawa na asilimia 69 ya mahitaji, hivyo kuleta upungufu wa lita 1,681,000. Mhandisi Ndomba aliishukuru Serikali kupitia Wizara ya Maji kwa kutenga fedha hizo na kutoa kibali cha utekelezaji wa mradi huo, ambao unalenga kumaliza kabisa mgao wa maji kwa wakazi wa Mbinga.
Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Mbinga,Mheshimiwa Kisare Makori, alisisitiza umuhimu wa utekelezaji wa mradi huo kufanyika kwa viwango vya juu na kwa wakati. Alizitaka kampuni husika kutoa ajira za muda kwa wananchi wanaoishi karibu na eneo la mradi, ili kuwawezesha kushiriki moja kwa moja kwenye uboreshaji wa huduma hiyo.
Amesema kuwa mradi huo utawezesha mji wa Mbinga kufikia asilimia 98.3 ya upatikanaji wa maji safi, hatua inayozidi lengo la Ilani ya Uchaguzi ya CCM la asilimia 95 kwa maeneo ya mijini.
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 S.L.P 74,SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: KERO PIGA 0800110174
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.