Chama cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Ruvuma kimefanya mkutano wa hadhara kwa ajili ya kuunga mkono azimio la mkutano mkuu wa chama hicho la kuwateua Dkt. Samia kuwa mgombea urais, Dkt. Emmanuel Nchimbi kuwa mgombea mwenza na Dkt. Mwinyi kuwa mgombea urais Zanzibar.
Akizungumza katika mkutano huo ambao umefanyika katika uwanja wa Matarawe mjini Songea, Mwenyekiti wa CCM mkoa wa Ruvuma, Komredi Oddo Mwisho, amesema wana kila sababu ya kuwaunga mkono wagombea hao kutekeleza ilani mbalimbali zilizobaki ili kuhakikisha wananchi wananufaika na rasilimali zilizopo.
Amewasisitiza wanachama kutotumia vibaya nafasi muhimu waliyopatiwa na Dkt. Samia ya kumteua Dkt. Nchimbi kuwa mgombea mwenza kwa kuwa wapo wanaotumia jina la mgombea kuwalaghai wanachama ili wajipatie kura badala yake wote waungane kusapoti juhudi za viongozi hao.
Hata hivyo amewataka wanachama wote awe kiongozi au wa kawaida hasa wanaojiona wanatosha kugombea uongozi kusubiri wakati na utaratibu utakaotolewa na hawatamvumilia yeyote ambaye ataleta jeuri na longolongo kuelekea uchaguzi mkuu utakaofanyika mwaka huu.
Naye Katibu wa CCM Mkoa wa Ruvuma, Mohammed Ally, amesema yeye kama mkurugenzi wa uchaguzi wa CCM Ruvuma anakemea chaguzi ambazo zimeanza kwa ajili ya kujaza wajumbe katika mashina na kuwataka kufuata utaratibu wa uchaguzi wa chama hicho.
Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma, Kanali Ahmed Abbas Ahmed, amesema ndani ya mkoa wa Ruvuma kuna miradi mingi inayotekelezwa lakini hivi sasa umepata bahati ya kuwa na mradi maalumu ambao mikoa mingine haijapata ambao ni kuteuliwa Dkt. Balozi Emanuel Nchimbi kuwa mgombea mwenza.
Mkutano mkuu maalum wa Chama cha Mapinduzi uliofanyika Dodoma kwa siku mbili Januari 18 na 19, 2025 ulimpitisha Dkt. Samia Suluhu Hassan kugombea urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia chama hicho, Balozi Dkt. Emmanuel Nchimbi kuwa mgombea mwenza pamoja na Dkt. Hussein Ali Mwinyi kuwa mgombea urais Zanzibar kuelekea uchaguzi mkuu wa Tanzania utakaofanyika mwaka huu.
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 S.L.P 74,SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: 0252602256
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.