Chama cha Walimu Tanzania (CWT) Manispaa ya Songea kimeipongeza Serikali ya awamu ya sita kwa kuhakikisha walimu wanapandishwa madaraja kwa wakati, wanapata daraja la mseleleko, na kulipwa viwango vipya vya mishahara.
Katibu wa chama hicho, Neema Lwila, alitoa pongezi hizo jana wakati akisoma risala ya walimu kwenye Mkutano Mkuu wa CWT uliofanyika katika ukumbi wa Anglikana mjini Songea.
Lwila alisema changamoto ya walimu waliokuwa na ajira ya pamoja kuachana kimadaraja imepata suluhisho baada ya Serikali kushirikiana na CWT kupitia Katibu Mkuu wa Ofisi ya Rais, Utumishi na Utawala Bora. Aliongeza kuwa juhudi hizo zinaendelea ili kuhakikisha walimu wote wanapata haki zao kwa wakati.
Aidha, Lwila alimpongeza Rais Samia Suluhu Hassan kwa kujenga zaidi ya shule 600 za msingi na sekondari, kuboresha miundombinu, kuajiri walimu wapya, na kuanza kulipa madeni ya walimu. Hata hivyo, alisisitiza kuwa bado walimu wanadai fedha nyingi na akaiomba Serikali kuwabana wakurugenzi wa halmashauri kuhakikisha mapato ya ndani yanatumika kulipa madeni yasiyohusiana na mishahara.
Afisa Elimu Msingi wa Manispaa ya Songea, Hossen Mghema, aliwataka walimu kuwa wazalendo kwa chama na kuiunga mkono Serikali kwa kuwa imefanya maboresho makubwa katika sekta ya elimu. Alibainisha kuwa mazingira ya kufundishia yameboreshwa, nyumba za walimu zimejengwa, na vifaa vya kufundishia vimetolewa ili kusaidia utoaji wa elimu bora.
Mghema alihimiza walimu na wanafunzi kutunza miundombinu ya shule ili idumu kwa muda mrefu kwa kuwa Serikali inatumia fedha nyingi kuitekeleza. Alisema Serikali inaendelea kupandisha madaraja ya walimu na kulipa madeni yao kulingana na sifa zao, akisisitiza kuwa juhudi hizo zinaonyesha dhamira ya dhati ya Serikali kuboresha maslahi ya walimu nchini.
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 S.L.P 74,SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: 0252602256
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.