Chama cha Walimu Tanzania (CWT) Manispaa ya Songea, mkoani Ruvuma, kimepongeza Serikali ya Awamu ya Sita kwa juhudi zake katika kuboresha maslahi ya walimu.
Juhudi hizo zinajumuisha kupandisha madaraja kwa wakati, kulipa viwango vipya vya mishahara, na kuhakikisha walimu wanapata daraja la mserereko.
Katibu wa CWT Manispaa ya Songea, Neema Lwila, alitoa pongezi hizo wakati wa Mkutano Mkuu wa chama hicho uliofanyika katika ukumbi wa Anglikana mjini Songea.
Alisema hatua hizo zimeleta faraja kwa walimu na kuimarisha hali yao ya kazi. Pia, alibainisha kuwa awali walimu waliokuwa na ajira ya pamoja walikuwa wakiachana kimadaraja bila sababu za msingi, lakini hali hiyo sasa imerekebishwa baada ya mazungumzo kati ya Serikali na CWT kupitia Katibu Mkuu wa Ofisi ya Rais – Utumishi na Utawala Bora.
Lwila alimpongeza Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuanzisha shule mpya zaidi ya 600 za msingi na sekondari, kuboresha miundombinu ya elimu kwa kukarabati madarasa na nyumba za walimu, pamoja na kuajiri walimu wapya.
Hata hivyo, alisisitiza kuwa licha ya Serikali kuanza kulipa madeni ya walimu, bado madeni hayo ni makubwa na yanapaswa kushughulikiwa kikamilifu.
Kwa upande wake, Afisa Elimu Msingi wa Manispaa ya Songea, Hossen Mghema, aliwataka walimu kuwa wazalendo na kuendelea kuiunga mkono Serikali kwa kuwa imefanya maboresho makubwa kwa walimu katika kipindi cha miaka minne.
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 S.L.P 74,SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: 0252602256
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.