Mkuu wa Wilaya ya Mbinga, Mhe. Kisare Makori, ametoa wito kwa taasisi za kidini kuwa mabalozi wa afya na lishe kwa kutoa elimu katika maeneo yao ili kutokomeza udumavu na kuimarisha afya bora kwa wananchi wa Wilaya ya Mbinga.
Wito huo umetolewa Februari 11, 2025, katika kikao cha tathmini ya mkataba wa lishe ngazi ya Halmashauri ya Wilaya ya Mbinga.
“Ndugu zangu viongozi, elimu hii ambayo tunaipata hapa tukawe mabalozi katika nyumba zetu za ibada. Sote tunatambua kuwa tukiwa na afya bora, tunaweza kutekeleza majukumu yetu bila wasiwasi,” alisema Mhe. Makori.
Aidha, ameihimiza Halmashauri ya Wilaya ya Mbinga kutumia kitengo cha Mawasiliano Serikalini ili kuendelea kuwafahamisha wananchi kuhusu utekelezaji wa afua za afya na lishe zinazofanywa na Serikali.
Kwa upande wake, Afisa Lishe wa Halmashauri ya Wilaya ya Mbinga, Elika Makwale, ameeleza kuwa jumla ya shilingi 33,437,500, sawa na 118.86%, zilitumika kutekeleza mkataba wa lishe kati ya Oktoba na Desemba 2024.
Askofu wa Kanisa la T.A.G Wilaya ya Mbinga, Mchungaji Exavery Mhagama, amepongeza juhudi hizo na kusisitiza kuwa lishe bora ni msingi wa afya njema. Ameahidi kuendelea kuwa balozi wa lishe kwa kutoa elimu ili kusaidia kutokomeza udumavu nchini.
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 S.L.P 74,SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: 0252602256
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.