Mkuu wa Wilaya ya Mbinga Mhe. Cosmas Nshenye amewataka watu wenye ulemavu kuchangamkia fursa ya mikopo inayotolewa na serikali kwa kuhakikisha wanarejesha fedha wanazokopa kwa wakati na kuiagiza Halmashauri ya Wilaya ya Mbinga kusimamia suala hilo kikamilifu ili fedha hizo ziweze kunufaisha watu wengine.
Mhe. Nshenye amesema hayo wakati wa kikao cha kutathmini changamoto zinazowakabili watu wenye ulemavu Wilayani Mbinga kilichofanyika leo Aprili 16 katika Ukumbi wa Safina uliopo Kigonsera, huku pia akiwataka watu hao kujiamini na kukubaliana na hali ya ulemavu waliyonayo kwa kusema watu wenye ulemavu wana haki zote na wajibu kama watu wengine.
Akizungumza kwenye kikao hicho, Mhe. Mkuu wa Wilaya amesema watu wenye ulemavu wanapaswa kujiona wenye bahati kwani serikali imewajali kwa kuwatengea asilimia maalumu ya fedha za mikopo licha ya watu hao kuwa na sifa nyingine za ziada za kupatiwa mikopo hiyo kupitia makundi ya vijana na wanawake.
Sambamba na hilo, pia Mhe. Nshenye ameitaka Halmashauri ya Wilaya ya Mbinga kuhakikisha suala la urejeshwaji wa fedha za mikopo linasimamiwa kikamilifu na kwa mujibu wa sheria na kuwaasa watu wenye ulemavu kuacha kulalamika na kufuta mawazo ya kujinyanyapaa huku akiwataka watu hao kuwa na fikra za kijasiriamali na kujipanga kurejesha fedha za mikopo kama inavyofanywa na wajasiriamali wengine wanaonufaika na mikopo ya 10% ya fedha za mapato ya ndani zinazotengwa na kutolewa na Halmashauri hiyo.
“Watu wa Halmashauri ukifika muda sheria hizi zitumike bila ubaguzi, hawa wote ni wajasiriamali na fedha hizi ni za watu wote..,hatuwezi kuwa na na vikundi visivyorejesha mikopo yao”. Ameongeza Mkuu huyo wa Wilaya.
Bw. Paschal Ndunguru, ambaye ni Afisa Maendeleo ya Jamii, Halmashauri ya Wilaya ya Mbinga amesema Halmashauri hiyo imekua ikitoaji mikopo ya wajasiriamali kwa vikundi vya watu wenye ulemavu kama sehemu ya jitihada zake za kuwezesha watu wenye ulemavu lakini vikundi hivyo vimekuwa na mwitikio hafifu wa kurejesha fedha hizo jambo linalopelekea kushindwa kuwezesha vikundi vingine vingi zaidi na kwa wakati.
Bw. Paschal amefafanua kuwa kwa miaka mitatu mfululizo kuanzia 2018/2019 hadi mwaka huu 2020/2021 Halmashauri ya Wilaya ya Mbinga imewezesha fedha jumla ya shilingi Milioni 98 kwa vikundi vya watu wenye ulemavu lakini fedha ambazo zimerejeshwa hadi sasa ni Milioni 30.6 pekee.
Awali wakizungumza mbele ya Mkuu wa Wilaya, viongozi wa Chama cha Watu Wenye Ulemavu (CHAWATA) na Shirikisho la Vyama vya Watu wenye Ulemamavu (SHIVYAWATA) Wilayani Mbinga wameshukuru kwa uwezeshwaji wa fedha ambao umekua ukifanywa na uongozi wa Halmashauri ya Wilaya ya Mbinga lakini pia wanaomba serikali kuendelea kuwajengea uwezo kwa kuwapa elimu ya ujasiriamali.
Pia viongozi hao wameiomba serikali kuona uwezekano wa kuweka ruzuku kwenye nyenzo na vifaa saidizi kwa watu wenye ulemavu ikiwa ni pamoja na kuweka watoa huduma ambao ni wakalimani wa lugha za alama kwenye maeneo ya kutolea huduma kama hospitali, mahakama, na vituo vya polisi.
Imeandikwa na:
Salum Said
Afisa Habari Halmashauri ya Mbinga
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: 0252602256
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.