MKUU wa Wilaya ya Nyasa mkoani Ruvuma Mheshimiwa Filberto Sanga amepiga marufuku uwepo wa Nyavu haramu na kuwaagiza viongozi wa vijiji, kata na Halmashauri pamoja na vyombo vya Ulinzi na usalama kuhakikisha hakuna uvuvi haramu unaoendelea, Wilayani Nyasa.
Ametoa katazo hilo katika kikao Cha Wadau wa uvuvi Cha kujadili Maendeleo ya uvuvi salama na endelevu chenye lengo la kuboresha Uvuvi Wilayani humo kilichofanyika katika Ukumbi wa Baylive mjini Mbamba bay.
“Tatizo la nyavu haramu ni la muda mrefu linaloathiri shughuli nzima za uvuvi na mazao yake katika ziwa Nyasa ambalo limesheneni Samaki wa aina mbalimbali wakiwemo samaki wa mapambo’’,alisema,
Mkuu wa Wilaya hiyo ametoa mwezi mmoja kuhakikisha Nyavu zote zinazoua mazalia ya samaki zinasalimishwa ambapo amesisitiza wote watakaoshindwa ndani ya muda huo watachukuliwa hatua za kisheria.
Amesisitiza wananchi kurudisha Nyavu hizo na kwamba msako wa nyumba hadi nyumba utaanza mara moja ili kuhakikisha nyavu hizo zinatokomezwa.
Amelitaja lengo kuu la kutokomeza uvuvi haramu ni kuboresha mazingira mazuri ya uvuvi ikiwa ni pamoja na kununua zana bora za uvuvi na kutoa mikopo Kwa wavuvi na wafanyabiashara ya Uvuvi.
Hata hivyo Mkuu wa Wilaya amewatoa hofu wananchi kwa kueleza kuwa Serikali imeandaa mpango wa kuboresha sekta ya Uvuvi ambao unatarajia kuanza kutekelezwa hivi karibuni.
Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Nyasa Khalid A.Khalif amesema atahakikisha anawasimamia kikamilifu watendaji wa Kata na vijiji ili kukabiliana na uvuvi haramu.
Wakizungumza katika kikao hicho wadau na viongozi, wamempongeza Mkuu wa Wilaya ya Nyasa Kupambana na Uvuvi haramu ambapo wameahidi kumuunga mkono na kutoa ushirikiano wa kutosha.
Wadau walioshiriki kwenye kikao cha uvuvi salama katika ziwa Nyasa ni waheshimiwa Madiwani, Wenyeviti vijiji, watendaji wa kata, Viongozi wa Wafanyibiashara za huduma katika uvuvi Wataalamu wa uvuvi, Wakuu wa Idara na Kamati ya Ulinzi na Usalama wilaya.
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 S.L.P 74,SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: 0252602256
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.