MKUU wa wilaya ya Tunduru mkoani Ruvuma Julius Mtatiro,amevunja ndoa na kufanikiwa kumrudisha shule mwanafunzi (jina linahifadhiwa)aliyekatishwa masomo baada ya kulazimishwa kuolewa na wazazi wake kwa mahali ya Sh.30,000.
Mwanafunzi huyo aliyechaguliwa kuendelea na masomo yake ya kidato cha tano katika shule ya sekondari ya wasichana Masasi,alifunga ndoa ya kimila mapema mwaka huu na kijana anayefahamika kwa jina la Mohamed Salum mkazi wa kijiji cha Muungano mara baada ya kumaliza masomo ya kidato cha nne mwaka jana.
Akizungumza mbele ya Waandishi wa Habari ofisini kwake mjini Tunduru alisema,kwa sasa mwanafunzi huyo amekabidhiwa katika taasisi moja wilayani humo inayojihusisha na malezi na kufadhili vijana.
Mtatiro alieleza kuwa,serikali ya wilaya inakamilisha taratibu za kumtafutia shule nyingine tofauti na aliyopangiwa hapo awali ili aweze kuendelea na masomo yake ya kidato cha tano.
Mtatiro alisema,ni kosa kisheria kwa wazazi au walezi kumuozesha mtoto anayepaswa kuendelea na masomo yake kwa sababu ni kinyume cha sheria na maadili.
Aliongeza kuwa,vitendo na tabia hiyo vimekuwa chanzo cha kuuwa ndoto za watoto wa kike katika maeneo mengi hapa nchini, na kuwaasa wazazi kuachana na mambo ya kizamani ya kuoza mabinti ambao wana nafasi ya kutoa mchango wao kwa Taifa.
“wale wote waliohusika katika kumuoza yule mwanafunzi watachukuliwa hatua mara tu taratibu za kisheria zitakapo kamilika,mambo ya namna hii yanapotokea lazima wanasheria wetu wakae na kuona namna gani ya kuendelea na hatua nyingine,sisi tunasubiri maelekezo nani anashitakiwe na kwa kosa lipi”alisema Mtatiro.
Alisema,serikali itaendelea kuwasimamia na kutoa ulinzi kwa watoto wa kike kama anavyopigia Rais Samia Suluhu Hassan ya kutaka watoto hao wanakuwa salama na wanaendelea na masomo yao ili waweze kutimiza ndoto za maisha yao.
Amewaonya wazazi wilayani humo,kutojarib kukatisha ndoto za watoto wa kike,badala yake kuhakikisha wanawapa nafasi na kuwasimamia kwa karibu ili wapate elimu bora itakayowasaidia katika maisha yao ya baadaye.
Alisema,elimu ndiyo ufunguo pekee utakaowapa njia wa kike kukabiliana na changamoto na mazingira ya kimaisha yanayokwenda kwa kasi kubwa ndani ya mfumo wa sasa wa Sayansi na Teknolojia na kuwataka wazazi kuwapa nafasi watoto wa kike ili kuendelea na masomo yao.
Baba mzazi wa mtoto huyo Athuman Ali,amefika ofisini kwa Mkuu wa wilaya na kuomba radhi kwa kumuoza mtoto wake akiwa bado mwanafunzi na kuishukuru serikali kwa hatua iliyochukua ya kumrudisha shule mtoto wake.
“nawaomba wazazi wenzangu ujinga niliofanya mimi na wao wasifanye,mimi na mke wangu tunajutia kitendo tulichofanya kumuozesha mtoto wetu aliyechaguliwa kuendelea na masomo yake,pia naiomba serikali itusamehe sana kwa kosa tulilofanya”alisema.
Amewataka wazazi wengine kuacha tabia hiyo badala yake kuwapa nafasi watoto wao kuendelea na masomo ili waweze kutimiza ndoto za maisha yao.
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 S.L.P 74,SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: 0252602256
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.