Moja ya vivutio kwenye eneo la Matchedje nchini Msumbiji ni uwepo wa gogo ambalo mwaka 1968 walikalia Rais Julius Nyerere wa Tanzania,Rais Edward Mondlane wa Msumbiji na Mkuu wa Majeshi alikuwa Samora Machel ambao walikaa kwenye gogo hilo kwa siku tano wakijadili namna ya kuikomboa nchi ya Msumbiji toka kwa wareno.
NCHI ya Tanzania wakati huo ikiwa chini ya uongozi wa Rais wa Awamu ya Kwanza Hayati Mwl.Julius Nyerere ilishiriki kikamilifu kwenye harakati za ukombozi kusini mwa Afrika.
Nchi ya Msumbiji ni miongoni mwa nchi ambazo hazitaisahau Tanzania ilivyotoa mchango wake hadi kusababisha nchi hiyo kupata uhuru wake toka kwa wareno mwaka 1975.
Alfonso Kaidavid ni Mhifadhi kwenye makumbusho ya Taifa ya Msumbiji yaliyopo Matchedje Jimbo la Niassa, anasema serikali ya Msumbiji imeamua kuanzisha makumbusho katika eneo hilo kutokana na kufanyika mkutano wa pili mwaka 1968 uliosababisha nchi hiyo kupata uhuru wake.
Anasema mkutano wa kwanza wa harakati za kuikomboa Msumbiji ulifanyika jijini Dar es salaam nchini Tanzania mwaka 1962 ukiongozwa na Rais Julius Nyerere wa Tanzania na viongozi waandamizi wa FRELIMO nchini Msumbiji ambao ni Edwardo Mondlane na Samora Machel.
Mhifadhi Kaidavid anasema Mkutano wa pili ulifanyika kwa siku tano katika eneo la Matchedje kuanzia Julai 20 hadi 25 mwaka 1968 na kwamba mkutano huo ulioongozwa viongozi waandamizi wakiwemo Rais Julius Nyerere wa Tanzania,Edwardo Mondlane na Samora Machel wa Msumbiji.
“Makumbusho haya tumeanzisha ili wanamsumbiji,watanzania na wageni wengine kutoka nchi mbalimbali waweze kujua ni namna gani nchi ya Msumbiji ilipambana katika kuikomboa nchi toka kwa wakoloni wareno ambao walitutawala kwa miaka mingi’’,anasisitiza Kaidavidi.
Picha hii ilipigwa katika kijiji cha Muhukuru Lilai wilayani Songea mkoani Ruvuma wakiwemo Rais wa Tanzania Mwl,Julius Nyerere,Rais wa Zambia Keneth Kaunda na Rais wa Msumbiji Samora Machel wakati wa harakati za ukombozi wa nchi ya Msumbiji
Anamtaja kiongozi wa FRELIMO hayati Edward Mondlane kwa kushirikiana na Samora Machel walipata mafunzo mbalimbali nje ya nchi ya Msumbiji namna ya kumfukuza mkoloni ili kuiacha Msumbiji huru.
Mhifadhi huyo anasema kabla ya kuamua kumwaga damu viongozi hao walijaribu kuzungumza na wareno ili wakubali kwa hiyari kutoa uhuru wa Msumbiji,hata hivyo ilishindikana ndipo waliamua kutumia njia ya bunduki.
Historia inaonesha kuwa wareno walifika nchini msumbiji mwaka 1498 na kwamba safari yao ilikuwa ni kwenda nchini India,hata hivyo waliamua kubaki Msumbiji,baada ya kubaini nchi hiyo ina utajiri mkubwa wa madini na meno ya tembo.
Akizungumzia vivutio vya utalii vilivyopo eneo hilo la kihistoria la Matchedje,Kaidavid anasema kwenye eneo hilo yamebakia masalia ya vibanda mbalimbali ambavyo viongozi wa kitaifa waliishi kwa siku tano kufanya mkutano wa pili mwaka 1968 uliozaa uhuru wa Msumbiji.
Moja ya vivutio kwenye eneo hilo ni uwepo wa gogo ambalo mwaka 1968 walikalia Rais Julius Nyerere wa Tanzania,Rais Edward Mondlane wa Msumbiji na Mkuu wa Majeshi alikuwa Samora Machel ambao walikaa kwenye gogo hilo kwa siku tano wakijadili namna ya kuikomboa nchi ya Msumbiji toka kwa wareno.
“Viongozi hao mwaka 1968 walijadili wakiwa wamekaa kwenye gogo hili ambalo hadi leo bado lipo likiwa vile vile bila kuoza,tumelihifadhi kama kumbukumbu muhimu kwenye harakati za ukombozi wa nchi ya Msumbiji’’,anasisitiza Mhifadhi huyo.
Maeneo mengine ambayo ni kivutio kwenye eneo hilo ni uwepo wa kibanda ambacho alilala kwa siku tano Rais wa Msumbiji Edwardo Mondlane mwaka 1968,pia kuna kibanda ambacho alilala Mkuu wa Majeshi Samora Machel kwa siku tano na kibanda ambacho walilala waandishi wa habari kwa siku tano.
Ukiachia harakati zilizoendelea nchini Msumbiji, eneo la Masonya lililopo katika Halmashauri ya Wilaya ya Tunduru mkoani Ruvuma nchini Tanzania lina utajiri wa utalii wa malikale na utambulisho wa Taifa,ingawa bado halifahamiki na wengi.
Eneo hilo lenye ukubwa wa ekari 100 lina vivutio adimu vya utalii wa malikale ikiwemo nyumba yenye namba A 10 ambayo walikuwa wanafikia na kuishi Marais Hayati Julius Nyerere wa Tanzania na Hayati Samaro Machel wa Msumbiji kuanzia 1966 wakati wa harakati za ukombozi Kusini mwa Afrika.
Mhifadhi wa Makumbusho ya Taifa ya Majimaji Bartazar Nyamusya anasema viongozi hao pia wakiwa katika nyumba hiyo,walitumia jengo dogo maalum lililopo jirani ya nyumba hiyo kama chumba cha mawasiliano yote na nchi zilizokuwa katika harakati za ukombozi kusini mwa Afrika.
Kutoka nyumba ya viongozi hao hadi jengo dogo la mawasiliano,lilijengwa handaki la chini kwa chini ambalo lipo hadi sasa lililokuwa linatumiwa na viongozi hao wa Tanzania na Msumbiji.
Historia inaonesha kuwa Rais wa sasa wa Msumbiji Pilipe Nyusi amesoma shule ya msingi FRELIMO iliyokuwepo katika eneo la Masonya ambaye alifika hapo mwaka 1970 akiwa na umri wa miaka nane.
Hata hivyo serikali hivi sasa inalitumia eneo la malikale la Masonya kwa shughuli za kielimu ambapo katika eneo hili imejengwa shule ya sekondari ya wasichana Masonya.
Kabla ya mwaka 1966,eneo la malikale la Masonya lilikuwa ni msitu ambapo katika mwaka huo ndipo serikali iliwapokea watu kutoka nchini Msumbiji na kuwakabidhi eneo hilo katika kipindi chote cha kupigania uhuru nchini Msumbiji.
Nurdin Seleman ni Mwenyekiti wa kijiji cha Masonya anasema kijiji hicho ilikuwa ni kambi ya wapigania uhuru wa nchi ya Msumbiji na kwamba eneo hilo lina malikale mbalimbali zilizokuwa zinatumiwa na wananchi wa Msumbiji
Anasema eneo hilo linatembelewa mara kwa mara na wananchi wa Msumbiji akiwemo Balozi wao ambapo serikali ya kijiji hicho inaendelea kuzitunza malikale hizo ambazo ni muhimu kwa vizazi vya sasa na vijavyo kwa maendeleo ya nchi zote mbili
Katika kipindi cha miaka kumi kuanzia 1966,wanawake toka nchini Msumbiji wamekuwa wanaishi katika eneo la Masonya,Umoja wa Wanawake wa Msumbiji unaojulikana kwa OMM ulianzia Masonya mwaka 1973.
Mkuu wa Wilaya ya Tunduru Julius Mtatiro anazitaja rasilimali adimu zilizopo katika eneo la malikale la Masonya kuwa ni majengo 13 ya FRELIMO na masalia ya kale ya nyumba za viongozi wa kitaifa ambao ni Hayati Julius Nyerere na Samora Machel.
Hata hivyo anasema mwaka 1975 baada ya nchi ya Msumbiji kupata uhuru wapigania uhuru hao walirudi nchini kwao na kuanzia mwaka 1990 Halmashauri ya Tunduru iliamua kuanzisha shule ya sekondari ya wasichana Masonya ambayo hadi kufikia mwaka 2014 inachukua wanafunzi wa kidato cha kwanza hadi cha sita.
Imeandikwa na Albano Midelo wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 S.L.P 74,SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: 0252602256
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.