Kamati Maalum ya Wataalamu wa Halmashauri ya Wilaya ya Mbinga imeanza zoezi la kufanya ufuatiliaji wa shughuli zinazofanywa na makampuni ya uchimbaji wa madini ya makaa ya mawe yaliyopo Wilayani Mbinga.
Kamati hiyo ambayo imeundwa na Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Mbinga inashughulikia masuala mbalimbali ikiwemo mwenendo mzima wa shughuli za uchimbaji na uchakataji wa makaa ya mawe, uzingatiaji wa masuala ya kimazingira, fidia ya ardhi na migogoro baina ya kampuni hizo na jamii inayozunguka maeneo ya migodi.
Timu hiyo imeanza kutekeleza majukumu yake Jumatano Mei 11 kwa kutembelea bandari kavu zote zilizopo Amani Makolo, Mkeso na Paradiso maeneo ambavyo pia ni vituo maalum vya uchakataji na mauzo ya makaa ya mawe vinavyoendeshwa na Kampuni za Mil Coal Ltd, Tan Coal energy Ltd, na Ruvuma Coal Ltd.
Kwa upande mwingine timu hiyo imetembelea na kukagua shughuli za uchimbaji wa madini ya makaa ya mawe kwenye mgodi unaoendeshwa na Kampuni ya Ruvuma Coal uliopo kijiji cha Paradiso na Sara.
Zoezi la ufuatiliaji wa shughuli za uchimbaji wa makaa ya mawe litaendelea tena Jumatatu Mei 17 kwa Kamati hiyo kutembelea Kijiji cha Sara ambapo watakutana na kuzungumza na wananchi wa vijiji vya Sara na Paradiso pamoja na wawakilishi wa Kampuni ya Ruvuma Coal ajenda kuu ikiwa ni suala la fidia kwa maeneo ya wananchi ambayo yapo ndani ya eneo la leseni mbili za uchimbaji wa makaa ya mawe zinazomilikiwa na Kampuni ya Ruvuma Coal.
Timu hii maalum ya ufuatiliaji wa shughuli za uchimbaji wa makaa ya mawe inaundwa na Mwenyeki wa Kamati, Bw. Paschal Zacharia (Afisa Maendeleo ya Jamii), Bw. Salum Said (Kaimu Afisa Mazingira) ambaye ni Katibu na wajumbe ambao ni Bi. Clementina Komba (Afisa Ardhi), Mponjoli Mwakalonge (Mwanasheria) na Waziri Geho ambaye pia ni Afisa Mtendaji Kata ya Ruanda.
Imeandikwa na Salum Said,
Afisa Habari, Mbinga D.C
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 S.L.P 74,SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: 0252602256
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.