HALMASHAURI YA MJI MBINGA ILIVYOFANIKIWA KUJENGA NYUMBA NANE ZA WATUMISHI KWA MILIONI 650
HALMASHAURI ya Mji wa Mbinga Mkoani Ruvuma, imetumia shilingi milioni 650 kwa ajili ya kutekeleza mradi wa ujenzi wa nyumba saba za wakuu wa Idara na nyumba moja ya Mkurugenzi
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri hiyo Grace Quintine amesema Halmashauri yake katika kipindi cha mwaka 2019/2020 ilipokea kiasi cha sh.milioni 350 kwa ajili ya nyumba saba za wakuu wa Idara na kwamba shughuli za utekelezaji zilianza Machi 26 ambapo hadi sasa mradi umefikia asilimia 75.
“Jumla ya shilingi milioni 284.374 zimetumika hadi sasa kati ya milioni 350,vifaa vyote vya viwandani kwa ajili ya utekelezaji wa mradi huo vimenunuliwa’’,alisema Quintine.
Amesema mradi ulitarajiwa kukamilika Juni mwaka huu,hata hivyo kutokana na changamoto ya kuchelewa kupokea bati ambazo ziliagizwa moja kwa moja kiwandani ALAF ilisababisha mradi kusimama kwa wiki mbili ambapo sasa mradi unatarajia kukamilika mwishoni mwa Julai mwaka huu.
Amesema miradi yote miwili inatekelezwa kwa kutumia force account ambapo kuna kamati tatu zinazosimamia mradi huu ikiwemo kamati ya ujenzi,kamati ya manunuzi na kamati ya mapokezi na ukaguzi.
Akizungumzia mradi wa ujenzi wa nyumba ya Mkurugenzi,Quintine amesema katika kipindi cha mwaka 2019/2020 Halmashauri iliidhinishiwa kutumia milioni 300 kwa ajili ya ujenzi wa nyumba ya Mkurugenzi ambayo ujenzi wake umefikia asilimia 65.
Amesema mradi huo pia unatekelezwa kwa force account na kwamba licha ya changamoto zilizochelewa mradi,hadi kufikia mwishoni mwa Julai mwaka huu,mradi wa nyumba ya Mkurugenzi unatarajia kukamilika kwa asilimia 100.
Kamati ya Siasa ya CCM Mkoa wa Ruvuma ikiongozwa na Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM Taifa Musa Homera ilikagua miradi yote miwili na kuridhishwa na utekelezaji wake ambao unakwenda kuondoa changamoto ya nyumba za kuishi kwa wakuu wa Idara na Mkurugenzi katika Halmashauri ya Mji Mbinga.
Homera ametoa rai kwa Halmashauri nyingine za Mkoa wa Ruvuma kuiga mfano wa Halmashauri hiyo ambapo sasa serikali itaondokana na kuwalipia wakuu wa Idara posho ya nyumba na fedha hizo kutumika katika shughuli nyingine za kuwaletea maendeleo wananchi wa Mbinga.
Imeandikwa na Albano Midelo
Afisa Habari wa Mkoa wa Ruvuma
Julai 10,2020
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 S.L.P 74,SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: 0252602256
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.