Katika kijiji cha Mbuji, wilayani Mbinga mkoani Ruvuma, ndipo unakutana na historia ya kipekee kwenye mawe ya kaburi la mviringo. Hii ni simulizi ya damu, ushindi, usaliti na heshima ya mwisho kwa shujaa wa kale wa Wamatengo.
KABURI LINALOZUNGUMZA
Katika kijiji cha Mbuji, yapo mawe yaliyopangwa kwa ustadi wa heshima. Hapo ndipo alipozikwa Chifu Kayuni Kapitangana Ndunguru Makita Mtawala wa kwanza wa Wamatengo na Amiri Jeshi Mkuu wa mapambano ya miaka ya moto dhidi ya Waarabu na Wangoni.
Chifu Makita si tu alikuwa kiongozi, bali alikuwa ngao ya taifa lake. Aliongoza mapambano makali kutoka mwaka 1824 hadi 1885, alipouawa kikatili kwa usaliti. Mwili wake ulizikwa ukiwa umekalishwa ishara ya heshima kwa mashujaa wa kale waliotangulia.
USHUJAA WA CHIFU MAKITA
Makita hakuwa tu mpiganaji jasiri bali pia mfanyabiashara mashuhuri aliyewavutia wengi kwa uwezo wa kipekee wa kuongoza.
Kwa mujibu wa Mheshimiwa Ngwatura Ndunguru aliyewahi kuwa Mbunge wa Mbinga na Afisa Wanyamapori,Makita alijijengea jina kwa hekima na ujasiri wake wa kupambana na hatari kubwa.
“Alianza kama shujaa, si chifu. Lakini mashujaa waliomzunguka walimtambua na kumpa mamlaka kwa sababu ya uwezo wake wa kuongoza na kushinda vita,” anasema Ndunguru.
USALITI ULIOGEUKA URITHI
Katika kile kinachoaminika kuwa hila ya Waarabu waliokuwa washirika wa kibiashara, Makita aliuawa kwa hadaa na kukatwa kichwa. Kichwa hicho kilikimbizwa kama ishara ya kushusha hadhi yake lakini haikufanikiwa.
Simulizi ya shujaa wa kike, Kingengi, ambaye kwa ujanja na imani za kiroho aliweza kukirudisha kichwa hicho kijijini, ni mfano halisi wa uzalendo na mapenzi kwa taifa. Aliwarubuni maadui kwa michezo ya jadi, akafanikiwa kuiba kichwa cha chifu wake waliokipora.
Usiku huohuo, wazee walikusanyika. Walikifunga kichwa kwenye kiwiliwili cha shujaa wao na kumzika kwa heshima ya kipekee, akiwa amekalishwa kwenye kaburi la mviringo. Vijana sita mashujaa, waliamua kuzikwa hai pamoja naye,wakiamini kuwa mtu mkubwa hawezi kwenda "ng’ambo ya pili" peke yake.
URITHI WA KISHUJAA ULIOFICHWA
Leo, zaidi ya miaka 140 baadaye, kaburi la Makita limesimama kijijini Mbuji kama ishara ya utambulisho wa Wamatengo. Mawe yaliyolizunguka yalipangwa upya mwaka 2004 na familia yake, kwa kushirikiana na viongozi wa kijiji wakati Ngwatura Ndunguru alipokuwa mbunge.
“Hadithi za mashujaa wetu bado hazijaandikwa vya kutosha. Serikali inapaswa kushirikiana na baraza la mila la Wamatengo kuhakikisha historia kama hii haipotei. Ni urithi wenye thamani kubwa ya kitaifa na kimataifa,” anasisitiza Ndunguru.
NI MUDA WA KUIFUKUA HISTORIA
Hadithi ya Chifu Makita si tu ya huzuni. Ni mwito wa kizalendo,sauti ya historia inayohitaji kusimuliwa upya. Mbinga inabeba kaburi lenye simulizi ya kiongozi aliyezikwa akiwa ameketi, akilindwa na mashujaa sita waliompenda mpaka mwisho.
Ni wakati wa Serikali, wanahistoria, na vijana wa sasa kuifufua simulizi hii na kuiweka katika vitabu vya historia, majukwaa ya kitaifa na maonesho ya utalii wa kiutamaduni.
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 S.L.P 74,SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: KERO PIGA 0800110174
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.