Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma, Kanali Ahmed Abbas Ahmed, amemkabidhi mkandarasi kutoka kampuni ya China National Aero Technology International Engineering Corporation (AVIC) mkataba wa ujenzi wa masoko ya kisasa ya Manzense A na B yatakayojengwa katika Kata ya Misufini, pamoja na kiwanda cha kuchakata mazao ya nafaka katika Kata ya Lilambo, Halmashauri ya Manispaa ya Songea.
Hafla ya makabidhiano ya mkataba huo imefanyika katika Kata ya Misufini, ambapo Kanali Ahmed amemuagiza mkandarasi kuhakikisha kuwa ujenzi huo unakamilika ndani ya muda uliopangwa, kwa kuwa wananchi wameusubiri kwa muda mrefu na wana matarajio makubwa.
Kwa kuzingatia thamani ya miundombinu hiyo, amewataka wananchi kushiriki kikamilifu katika kulinda rasilimali zote zilizoandaliwa kwa ajili ya ujenzi huo, na kuhakikisha kuwa masoko hayo yanatunzwa ipasavyo mara baada ya kukamilika.
Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Songea, Wakili Bashir Muhoja, ameeleza kuwa jumla ya shilingi bilioni 22.9 zitatumika katika ujenzi wa masoko hayo pamoja na kiwanda cha kuchakata mazao ya nafaka ambapo Kampuni ya China National Aero Technology International Engineering Corporation (AVIC) ndiyo iliyopatiwa zabuni ya kutekeleza mradi huo.
Amebainisha kuwa mradi huo unatarajiwa kuanza rasmi tarehe 15 Julai 2025 na kukamilika ifikapo 15 Julai 2026 na utekelezaji wake unatarajiwa kuleta matokeo chanya kwa kuboresha mazingira ya biashara, kuongeza thamani ya mazao ya wakulima, na kutoa fursa za ajira kwa wananchi wa Songea na maeneo ya jirani.
Kwa upande wa Sekretarieti ya Mkoa, Jumanne Mwankhoo, akimwakilisha Katibu Tawala wa Mkoa wa Ruvuma, ameeleza kuwa kwa kuzingatia maelekezo ya Waziri wa TAMISEMI, mradi huo utasimamiwa kwa karibu ili kuhakikisha unakamilika kwa wakati na kwa viwango vinavyotakiwa.
Mkandarasi kutoka kampuni ya AVIC, Bw. Kevin Long, ameahidi kukamilisha mradi huo kwa wakati na kushirikisha wananchi katika ajira mbalimbali zitakazopatikana wakati wa ujenzi.
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 S.L.P 74,SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: KERO PIGA 0800110174
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.