HALMASHAURI ya Wilaya ya Namtumbo mkoani Ruvuma imepata hati safi katika matokeo ya ukaguzi ambao ulifanywa kwa mwaka wa fedha ulioishia Juni 30,2021.
Akizungumza katika kikao maalum cha Baraza la Madiwani cha kujadili taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali CAG katika Halmashauri ya Namtumbo,Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Brigedia Jenerali Wilbert Ibuge amewapongeza watumishi na Baraza la madiwani kwa kusahihisha makosa walioyafanya mwaka 2019/2020 ambapo Halmashauri hiyo ilipata hati yenye mashaka.
RC Ibuge amesema hati yenye mashaka katika kipindi hicho ilileta doa kwenye rekodi za kupata hati safi ambapo hivi sasa Halmashauri hiyo imerejea kwenye mstari wa kupata hati safi.
“Napenda sasa nitoe maelekezo kama sehemu ya dira katika kujihakikishia kuwa Namtumbo inaendelea kupata hati safi kwa kuhakikisha hoja zote zilizosalia zifungwe,zuieni kujirudia hoja,wakuu wa Idara washiriki ipasavyo kuandaa majibu ya hoja na utekelezaji wa mapendekezo ya CAG’’,alisisitiza Ibuge.
Mkuu wa Mkoa pia ameagiza Halmashauri kuchukua mapema hatua za kinidhamu kwa watumishi wanaozalisha hoja ili isionekane ni jambo la kawaida na kwamba upotevu wa mapato katika Halmashauri na vyanzo vya upotevu vidhibitiwe na hatua zichukuliwe kwa wahusika.
RC Ibuge pia ameagiza kuwepo umakini mkubwa katika utekelezaji wa sheria,kanuni na taratibu za manunuzi na kwamba Halmashauri iendelee kulipa madeni mbalilmbali ya wazabuni kwa wakati ili iweze kujiendesha kwa tija.
Mkuu wa Mkoa pia ameipongeza Halmashauri ya Namtumbo kwa kuchangia kwa asilimia 87.5 mfuko wa wanawake,vijana na watu wenye ulemavu ambapo wameweza kuchangia shilingi milioni 83.
Hata hivyo amesema Halmashauri ya Namtumbo katika mwaka wa fedha 2020/2021 imeweza kukusanya mapato ya ndani kwa asilimia 82.62 ya lengo la kukusanya Zaidi ya shilingi bilioni 1.77 hivyo kufanikiwa kukusanya Zaidi ya shilingi bilioni 1.46.
Katika hatua nyingine Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma amemuagiza Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo kuendelea kuwasimamisha kazi watumishi ambao ni Afisa Manunuzi Samson Manjale na Afisa Maendeleo ya Jamii Pelesta Mugusha ili kupisha uchunguzi unaoendelea kufanywa na Tume maalum.
Brigedia Jenerali Ibuge amemuagiza Mkuu wa TAKUKURU Mkoa wa Ruvuma kufanya uchunguzi mara moja kuhusiana na tuhuma zinazowakabili watumishi hao ambapo amemtaka Mganga Mkuu wa Wilaya ya Namtumbo kutoa ushirikiano katika uchunguzi wa TAKUKURU.
Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma ameanza vikao maalum vya Baraza la madiwani katika Halmashauri zote nane ili kujadili taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za serikali.
Imeandikwa na Albano Midelo
Afisa Habari Kitengo cha Mawasiliano Serikalini Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma
Juni 13,2022
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 S.L.P 74,SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: 0252602256
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.