HALMASHAURI ya wilaya ya Songea mkoani Ruvuma,imepokea kiasi cha Sh.milioni 380 kutoka Serikali kuu kwa ajili ya kujenga vyumba 19 vya madarasa kwenye shule shikizi zilizojengwa kwenye maeneo yenye mazingira magumu ya kupata elimu kwa wanafunzi.
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri hiyo Neema Maghembe alisema,fedha hizo zimetumika kujenga jumla ya shule mpya tano za msingi ikiwamo shule ya Lihuhu ili kuwanusuru watoto wenye umri wa kuanza shule kukosa haki ya kupata elimu.
Maghembe alisema,awali wanafunzi wanaotoka katika kijiji cha Lihuhu walilazimika kutembea umbali wa km 7 kwenda kijiji cha Lilahi kufuata shule, hivyo kusababisha baadhi yao kukatisha masomo.
Alisema,katika kijiji hicho ambacho mwanzo kilikuwa kama kitongoji cha kijiji mama cha Lilahi,serikali imejenga jumla ya madarasa matatu kwa gharama ya Sh.milioni 60 ikiwa ni mkakati wake wa kuimarisha na kuboresha miundombinu ya elimu.
Alisema,baada ya kukamilika kwa ujenzi wa vyumba hivyo,sasa wanafunzi wamekuwa na mazingira mazuri ya kujisomea na walimu kuwa na muda mzuri ya kufundisha ikilinganishwa na awali ambapo kulikuwa na madarasa ya miti yaliyojengwa na wananchi.
Maghembe alitaja shule zilizojengwa kupitia fedha hizo ni Jenista Mhagama, ambapo serikali imejenga vyumba vitatu kwa gharama ya Sh.milioni 60 na shule ya msingi Lunyele madarasa matatu kwa Sh.milioni 60.
Shule nyingine zilizonufaika na fedha hizo ni Mhimbasi iliyopata madarasa matano kwa gharama ya Sh.milioni 100 na kata ya Kizuka ambapo imejengwa shule mpya yenye madarasa Matano kwa gharama ya Sh.milioni 100.
Alisema,serikali inaendelea kufanya juhudi kubwa kuhakikisha kila mtoto mwenye umri wa kuanza elimu ya awali,msingi na sekondari anapata elimu na kuwaomba wazazi,walezi na jamii kwa ujumla kushiriki na kujitolea nguvu zao kujenga na kuboresha miundombinu ya elimu.
Baadhi ya walimu wa shule hizo, wameipongeza Serikali kwa jitihada zake za kujenga na kuboresha miundombinu ya elimu katika maeneo mbalimbali.
Mwalimu mkuu wa shule ya Lihuhu Simon Pascal alisema kuwa, madarasa hayo mapya yamehamasisha sana wanafunzi kuhudhuria masomo na kukomesha tatizo la utoro na kurudisha morali ya kufundisha kwa walimu.
Mwalimu Pascal alisema,baada ya kujengwa madarasa mpya hata idadi ya watoto wanaoanza darasa la kwanza imeongezeka kutoka 20 mwaka wa masomo 2020/2021 hadi 45 kwa mwaka wa masomo 2021/2022.
Mwalimu wa shule ya msingi Lunyele kata ya Muhukuru Silvesta Ngumba,ameiomba serikali kupitia Halmashauri ya wilaya kuwasaidia walimu wanaofanya kazi kwenye maeneo yenye mazingira magumu kwa kutoa motisha na kuboresha mazingira yao.
Alisema,licha ya serikali kujenga vyumba vipya vya madarasa kwa ajili ya kuboresha mazingira ya kujifunza na kufundishia,hata hivyo kwa upande wa walimu bado wanakabiliwa na mazingira magumu.
Alisema,changamoto kubwa hasa ni makazi kwani katika shule hiyo kuna walimu watano ambao wanaishi kwenye nyumba moja ambayo haina hadhi ya kuishi mtumishi wa umma.
Aidha alisema, hata wanapohitaji kufika makao makuu ya Halmashauri ya wilaya au Songea mjini, wanalazimika kutumia zaidi ya shilingi 50,000 kama nauli,hivyo ameiomba serikali kuwaangalia kwa jicho la huruma watumishi waliokubali kufanya kazi kwenye mazingira hayo.
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 S.L.P 74,SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: 0252602256
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.