HALMASHAURI ya Wilaya ya Songea mkoani Ruvuma imekuwa ya kwanza kimkoa katika matokeo ya mashindano ya mbio za Mwenge wa Uhuru mwaka 2019.
Hayo yamesemwa na Katibu Tawala Msaidizi Serikali za Mitaa mkoani Ruvuma Joel Mbewa akitoa taarifa ya Mbio za Mwenge wa Uhuru mwaka 2019 katika kikao cha maandalizi ya mbio za Mwenge wa Uhuru mwaka 2020 kilichofanyika kwenye ukumbi wa Manispaa ya Songea na kushirikisha Halmashauri zote nane za Mkoa wa Ruvuma.
Licha ya kushika nafasi ya kwanza kimkoa,Mbewa amesema Halmashauri hiyo pia katika Mbio za Mwenge wa Uhuru 2019,imekuwa ya nane kikanda na nafasi ya 42 kitaifa.
Mbewa ameitaja Halmashauri ya pili kimkoa kuwa ni Halmashauri ya Wilaya ya Mbinga,Halmashauri ya Mji Mbinga imeshika nafasi ya tatu,Nyasa ni ya nne,Tunduru ya tano,Namtumbo ya sita,Madaba ya saba na ya mwisho ni Halmashauri ya Manispaa ya Songea.
Hata hivyo Mbewa ameutaja mkakati wa mwaka 2020 katika mbio za Mwenge wa Uhuru mkoani Ruvuma ni kuhakikisha kuwa Mkoa unaingia katika mikoa mitano bora.
Mbio za Mwenge wa Uhuru mwaka 2020 zinatarajiwa kuzinduliwa Mkoa wa Kusini Magharibi Zanzibar Aprili pili,2020,ambapo katika Mkoa wa Ruvuma Mwenge wa Uhuru unatarajia kukimbizwa kuanzia Mei 12,2020 hadi Mei 19,2020.
Imeandikwa na Albano Midelo
Afisa Habari Mkoa wa Ruvuma
Machi 9,2020
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 S.L.P 74,SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: 0252602256
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.