SERIKALI kupitia kitengo cha kifua kikuu na ukoma Hospitali ya wilaya Tunduru mkoani Ruvuma,imeanza msako wa kuwasaka waganga wa tiba asili wanaowarubuni wagonjwa wa kifua kikuu wasiendelee kutumia dawa za Hospitali ili watumie dawa za asili kwa lengo la kujipatia fedha.
Mratibu wa kifua kikuu na ukoma wa wilaya ya Tunduru Dkt Mkasange Kihongole alisema,msako huo unakwenda sambamba na kuwatafuta watu wote waliobainika kuwa na maambukizi ya ugonjwa huo walioanzishiwa matibabu lakini wameacha kwenda Hospitali na kutumia dawa kwa sababu zisizofahamika.
Dkt Kihongole amesema hayo jana,wakati wa zoezi la kuwasaka waganga hao na wagonjwa wa kifua kikuu katika kijiji cha Nandembo,huku baadhi ya wagonjwa wamekutwa katika kilinge cha mganga wa tiba asili Mohamed Heja wakipatiwa dawa za asili.
Aidha msako huo unawahusisha wataalam wa kitengo cha kifua kikuu na ukoma wa Hospitali hiyo na watendaji wa vijiji na kata kama njia rahisi ya kuwapata wagonjwa waliokatisha kumeza dawa kama hatua ya kudhibiti kuenea kwa ugonjwa huo.
Alisema,lengo la msako huo ni kuwapata wagonjwa waliobainika kuwa na kifua kikuu na kuanzishiwa matibabu lakini kutokana na sababu zisizojulikana hawafiki Hospitali kupata ushauri na kuendelea kumeza dawa,jambo ambalo ni hatari kwao na jamii inayowazunguka.
Alisema,wilaya ya Tunduru inatajwa kuwa na maambukizi makubwa na wagonjwa wengi wa kifua kikuu,kwa hiyo zinahitajika nguvu za pamoja ili kuinusuru jamii kupata ugonjwa huo unaoongoza kupoteza maisha ya watu wengi hapa nchini.
Alisema,kifua kikuu ni hatari kwa kuwa ni rahisi sana kwa mtu mwenye ugonjwa huo ambaye bado hajaanzishiwa matibabu au kuacha kumeza dawa kuambukiza mtu mwingine kwa haraka zaidi kupitia mfumo wa hewa.
Dkt Kihongole alisema,kutokana na ukubwa wa tatizo hilo ndiyo maana serikali na wadau wengine imewekeza nguvu kubwa katika kupambana na ugonjwa huo ambapo matibabu yake utolewe bure katika zahanati,vituo vya afya na Hospital zote hapa nchini.
Alisema,serikali inatumia gharama kubwa katika kupambana na maradhi hayo kwa kufanya kampeni za mara kwa mara za uelimishaji,uibuaji na uchunguzi ambazo zimesaidia kuwapata wagonjwa wa kifua kikuu ambao walibaki majumbani bila kupata tiba sahihi.
Ameagiza wagonjwa wa kifua kikuu waliokutwa katika kilinge hicho warudishwe Hospitali kuendelea na matibabu,na kuwataka waganga wa tiba asili kuacha tabia ya kukumbatia wagonjwa wanaohitaji kupatiwa tiba za kitaalam.
Alisema,serikali inatambua shughuli za tiba asili zinazofanywa na waganga hao,hata hivyo ni muhimu kunatoa tiba sahihi,kuacha udanganyifu kwa wateja wao, kuhakikisha wanafuata sheria na kuepuka kuchochea migogoro katika jamii.
Dkt Mkasange amewaagiza watendaji wa vijiji na kata,kuwakamata na kuwafikisha kwenye vyombo vya sheria waganga wa tiba asili wanaofanya kazi katika maeneo yao bila kufuata sheria kwa kutokuwa na vibali vya serikali na kupiga ramli chonganishi.
Mtendaji wa kata ya Nandembo Zuber Ngoma,amewataka wananchi kujiridhisha kwanza kabla ya kwenda kwa waganga wa tiba asili ambao baadhi wameonekana ni wababaishaji na matapeli wanaofanya kazi ili kujipatia kipato
Alisema,mara kwa mara serikali imekuwa ikitoa tahadhari kwa wananchi kuhusu hatari ya kukimbilia kwa waganga wanaotumia shida na udhaifu wao kuwaibia,lakini changamoto kubwa ni imani potofu kwa jamii kwenye masuala ya asili.
Kwa upande wake Mganga wa tiba asili aliyekutwa na wagonjwa wa kifua kikuu katika kilinge chake Yasin Heja alijitetea kuwa,kwa sasa yuko kwenye mafunzo kwa vitendo ambapo anategemea kupata vibali mwezi Julai.
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: 0252602256
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.