Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Christina Mndeme amekagua hospitali ya wilaya ya Namtumbo ambayo imeanza kuhudumia wananchi na serikali imepeleka madaktari.
Akizungumza baada ya kukagua hospitali hiyo,Mndeme kwa niaba ya wananchi wa Namtumbo amemshukuru Rais kwa kutoa fedha kiasi cha shilingi bilioni 1.5 zilizotumika kutekeleza ujenzi wa hospitali hiyo.
Amesema kabla ya Rais kutoa fedha hizo,wilaya ya Namtumbo ilikuwa haina hospitali ya wilaya hivyo serikali kwa kuwajali wananchi na kuboresha sekta ya afya iliamua kujenga hospitali ya wilaya iliyokamilika.
“Nawapongeza madiwani na wataalam wote kwa kusimamia ujenzi wa hospitali hii na kufanikiwa kujenga majengo tisa na kiasi cha fedha iliyobaki kinatumika kujenga jengo la kumi na ujenzi wa walk way’’,alisema.
Kaimu Mganga Mkuu Halmashauri ya Namtumbo Dr.Godwin Luta amesema hivi karibuni wanatarajia kuanza kutoa huduma za kulaza wagonjwa.
Luta amesema Mei 30 mwaka huu wamepokea kiasi cha shilingi milioni 300 toka serikalini, kwa ajili ya kuendeleza uboreshaji wa eneo la hospitali ya wilaya na kwamba tayari wameanza kutoa baadhi ya huduma za hospitali kwa wananchi.
Hata hivyo amesema wanatarajia hivi karibuni kuanza kulaza wagonjwa na kwamba wamenunua dawa na vifaa tiba ikiwemo magodoro,vitanda na mashuka 50 ili huduma ya malazi iweze kuanza mara moja.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Namtumbo Venance Nachimbinya amesema wamejenga walk way ya mfano yenye urefu wa meta 150 na kwamba majengo karibu yote yametekelezwa kwa asilimia 99 ndiyo maana huduma zimeanza kutolewa katika hospitali hiyo.
Imeandikwa na Albano Midelo
Afisa Habari wa Mkoa wa Ruvuma
Juni 11,2020
Namtumbo
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: 0252602256
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.